Ghasia, ajali ya moto katika jela nchini Venezuela vyaua watu 68
(last modified Thu, 29 Mar 2018 15:00:48 GMT )
Mar 29, 2018 15:00 UTC
  • Ghasia, ajali ya moto katika jela nchini Venezuela vyaua watu 68

Kwa akali watu 68 wamepoteza maisha katika vurugu zilizozuka katika gereza moja nchini Venezuela na kusababisha kutokea kwa mkasa wa moto.

Duru za habari zinasema matukio hayo yalijiri hapo jana Jumatano, baada ya wafungwa katika gereza moja lililoko mjini Valencia, makao makuu ya jimbo la Carabobo kaskazini mwa nchi, kuzusha ghasia kwa lengo la kutaka kutoroka jela.

Carlos Nieto, mkuu wa gereza hilo amesema baadhi ya wafungwa waliteketea kwa moto hadi kufa na wengine wakafariki dunia kwa kukosa hewa baada ya moto huo kuanza kuchoma magodoro kwenye jela hiyo. Amesema baadhi ya wafungwa hao waliuawa walipojaribu kuwapokonya silaha walinzi wakiwa na nia ya kutoroka jela.

Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, Tarek William Saab amethibitisha kutokea vurugu hizo kaskazini mwa jimbo la Carabobo, huku akisisitiza kuwa moto huo uliwashwa kwa makusudi.

Wafungwa waliofurika kwenye jela moja ya Venezuela

Amebainisha kuwa, miongoni mwa walioaga dunia kwenye tukio hilo ni wanawake wawili ambao walikuwa wameenda kuwatembelea ndugu zao katika jela hiyo, na kwamba waendesha mashtaka wanne wa serikali wametwikwa jukumu la kuchunguza tukio hilo.

Matukio ya namna hii yamekuwa yakishuhudiwa mara kwa mara kwenye magereza ya Venezuela, huku wafungwa nchini humo wakikabiliwa na hali mbaya haswa kukosa mahitaji ya msingi na magereza kujaa kupita kiasi.

 

Tags