Vita vya ujasusi vya Uingereza dhidi ya Russia
Kufuatia kufukuzwa wanadiplomasia wa Russia katika nchi 26 duniani, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ya Uingereza ametangaza kuwa, nchi hiyo imechukua hatua isiyo na mfano na kuzipa nchi waitifaki taarifa za majasusi wake zinazohusiana na faili la kupewa sumu ya kemikali jasusi wa zamani wa Russia katika eneo la Salisbury huko kusini mwa London.
Kutolewa kwa taarifa hizo za kipelelezi kumetayarisha mazingira ya kufukuzwa wanadiplomasia wa Russia katika nchi za Magharibi. Hadi sasa nchi 26 zimewafukuza wanadiplomasia wanaokaribia 150 wa Russia.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amesema tukio hilo ndilo kubwa zaidi katika historia la kufukuzwa idadi kubwa ya wanadiplomasia wa Russia katika nchi za Magharibi. Vilevile Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza, Boris Johnson anasema: Kufukuzwa wanadiplomasia wa Russia katika nchi za Magharibi ni tukio muhimu katika uhusiano wa Magharibi na Moscow na ni dhoruba kubwa itakayolilazimisha shirika la ujasusi la Russia kutumia miaka mingi ili kuondokana na athari zake mbaya.
Serikali ya kihafidhina ya London inaamini kuwa, kufukuzwa wanadiplomasia karibu 150 wa Russia katika nchi za Magharibi na washirika wao kutatoa pigo kubwa kwa taasisi na vyombo vya ujasusi wa nje vya nchi hiyo kwa sababu Moscow itakuwa imepoteza maajenti wake wengi wa ujasusi katika nchi hizo.
Serikali ya Uingereza ambayo imekataa wito wa mara kwa mara wa Russia inayotaka ipewe ushahidi wa kuhusika Moscow katika kile kinachodaiwa ni njama ya kutaka kumuua kwa sumu jasusi wa zamani wa nchi hiyo nchini Uingereza, sasa inafanya vita vya kipropaganda ikidai kuwa imetoa ushahidi huo kwa waitifaki wake.
Hapa linajitokeza swali kwamba, kama kweli London ina ushahidi madhubuti unaoothibitisha kuwa Moscow ilihusika katika njama hiyo, kwa nini isiuoneshe waziwazi kwa jamii ya kimataifa na kuilazimisha Russia kutoa majibu? Mbinu iliyotumiwa na maafisa wa serikali ya Uingereza kueleza kuwa wamekabidhi ushahidi huo kwa nchi waitifaki inaonesha kuwa, matamshi hayo ni wimbi la kipropaganda linalofanyika kwa shabaha ya kuanzisha vita vya kisaikolojia na kinafsi dhidi ya Russia.
Kwa kutilia maanani historia na utendaji wa Uingereza, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanatilia shaka madai kuwa Russia ilihusika katika njama ya kumuua jasusi wake wa zamani nchini Uingereza, Sergei Skripal na binti yake, Yulia kwa kutumia sumu ya kemikali. Mbali na hayo inaonekana kuwa madai hayo pia yanatumiwa na London na waitifaki wake kwa ajili ya kuibana zaidi Rusia na kuiwekea vikwazo zaidi vya kimataifa ikiwa ni pamoja na kususia fainali za Kombe la Dunia la Soka mwaka 2018 nchini Russia.
Ni vyema pia kukumbusha kwamba, nchi za Poland, Iceland, Denmark, Sweden, Australia na Japan ambazo zilizopata tiketi ya kushiriki katika mashindano hayo zimetangaza kuwa maafisa wao wataungana na Uingereza katika kususia mwaliko wa kushiriki katika sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia.
Akijibu harakati za Uingereza za kuwataka washirika wake wasusie sherehe hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Russia, Nikita Simonyan amesema: "Wamagharibi walikuwa wakidai kuwa michezo inapaswa kutenganishwa na siasa lakini sasa wanatumia Kombe la Dunia la Soka kama silaha ya kisiasa na kipropaganda dhidi ya mataifa mengine."