Apr 02, 2018 04:36 UTC
  • Erdoğan amwita Netanyahu 'gaidi' na aitaja Israel 'dola la kigaidi'

Matamshi makali ya ukosoaji yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina yamepelekea kuibuka vita vya maneno kati yake na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Kufuatia ukosoaji wa Netanyahu kwa Erdogan kutokana na operesheni zinazotekelezwa na jeshi la Uturuki katika eneo la Afrin kaskazini magharibi mwa Syria, Rais wa Uturuki amejibu mapigo kwa kumhutubu Netanyahu kwa kusema: "Anasema askari wetu wanakandamiza watu Afrin. Netanyahu, wewe ni dhaifu mno, ni duni mno. Sisi tunakabiliana na magaidi, lakini nyinyi hamko hivyo. Nyinyi ni dola la kigaidi". Rais wa Uturuki aidha amemwita Waziri Mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni "ghasibu" wa ardhi za Palestina na kuongezea kwa kusema: "Wewe ni gaidi pia. Historia inarekodi uliyoyafanya kwa Wapalestina wote madhulumu".

Rais wa Uturuki ameendelea kueleza kuwa, hakuna haja ya kuzitolea ufafanuzi dhulma zinazofanywa na jeshi la Israel, kwa sababu kila mtu anajua jinai zinazofanywa na utawala huo wa kigaidi katika Ukanda wa Gaza na Baitul Muqaddas.

Kijana mdogo wa Kipalestina aliyejeruhiwa na askari wa Kizayuni akikimbizwa ili kuokoa maisha yake

Siku ya Ijumaa iliyopita Wapalestina zaidi ya elfu kumi walifanya maandamano makubwa katika mpaka wa Ukanda wa Gaza chini ya anwani ya "Haki ya Kurejea" . 

Siku hiyo jeshi la utawala wa Kizayuni lilituma wanajeshi zaidi ya elfu tatu katika eneo hilo na kuanza kuwafyatulia risasi, kuwanyunyizia gesi ya kutoa machozi na kuwatupia maguruneti waandamanaji. Katika vurumai hizo utawala huo haramu uliwaua shahidi Wapalestina 17 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 1400.

Maandamano ya kwanza ya "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu miaka 42 iliyopita tarehe 30 Machi mwaka 1976 kulaani hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina.../

 

 

 

Tags