Bajeti ya vikosi vya kusimamia amani vya Umoja wa Mataifa yapasishwa
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeafiki na kupasisha bajeti ya vikosi vya kusimamia amani vya umoja huo katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa, nchi wanachama wa umoja huo zimepasisha kiasi cha dola bilioni 6.7 kwa ajili ya askari wa kusimamia amani.
Inaelezwa kuwa, kiwango hicho ni kipungufu kwa dola milioni 122 ikilinganishwa na bajeti iliyokuwa imependekezwa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa na ni kipungufu kwa dola milioni 60 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana.
Kwa sasa Umoja wa Mataifa una takribani askari laki moja wa kusimamia amani katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.
Ripoti zaidi zinaeleza kuwa, vikosi vya kusimamia amani vya Umoja wa Mataifa vyenye gharama kubwa ni vile vilivyoko Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Mali ambapo kila moja kati ya vikosi hivyo kinagharimu zaidi ya dola bilioni moja kwa mwaka.
Nikki Haley, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ametoa wito wa mataifa mengine kuwa na ushiriki zaidi katika kudhamini bajeti ya vikosi hivyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Marekani imetangaza kuwa, itapunguza kwa asilimia 25 udhamini wa fedha za vikosi vya kusimamia amani vya Umoja wa Mataifa.