Siku ya Kimataifa ya Shujaa Mandela Yaadhimishwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46871-siku_ya_kimataifa_ya_shujaa_mandela_yaadhimishwa
Dunia imeadhimisha Siku ya Nelson Mandola ikiwa ni mwaka wa 100 tangu kuzaliwa kwa Rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 19, 2018 03:07 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Shujaa Mandela Yaadhimishwa

Dunia imeadhimisha Siku ya Nelson Mandola ikiwa ni mwaka wa 100 tangu kuzaliwa kwa Rais wa kwanza Mwafrika wa Afrika Kusini

Katika kuadhimisha siku hiyo Umoja wa Mataifa umesema Hayati Mandela anakumbukwa kwa harakati zake za kupigania haki na usawa na zaidi ya yote kuendelea kuleta msukumo duniani kupitia mifano yake ya  ujasiri na huruma.

Katika ujumbe wake wa siku hii inayoadhimishwa tarehe 18 Julai kila mwaka, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema. “Nelson Mandela alikuwa mateka kwa miaka mingi, lakini hakuwa mfungwa wa yaliyomfika. Badala yake  alitumia nguvu zake katika kusameheana pamoja na kuona hali ya baadaye ya   Afrika Kusini yenye amani, makabila tofauti na ya kidemokrasia.”

Guterres ameongeza kuwa  ingawa amefariki dunia lakini bado mchango wake unatambulika akisema, “Hakuna mtu ambaye katika historia yake amewahi kufanya mengi kuchochea ndoto za watu wengi na kuwafanya watekeleze kivitendo ndoto zao kama Mandela. 

Maadhimisho ya siku ya 18 Julai yaliidhinishwa na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Novemba 2009 ambalo lilitangaza siku hii kama ya kimataifa na hiyo ni kutokana na kazi zake za kupigania amani na uhuru.

Mandela akitambulika pia kama Madiba, anakumbukwa kwa kujitolea kwake kutatua migogoro, kuboresha uhusiano baina ya watu wenye asili na rangi tofauti, kusamehe wengine, kuboresha haki za binadamu, kuendeleza usawa wa kijinsia, kupambana dhidi ya umasikini na mengine mengi.