Jumatano, tarehe 11 Februari, 2026
Leo ni Jumatano tarehe 22 Sha'ban 1447 Hijria sawa na Februari 11 mwaka 2026.
Katika siku kama ya leo miaka 859 iliyopita alifariki dunia mfasiri, faqihi, mpokezi wa Hadithi na alimu mkubwa wa Kiislamu Ibn Shahrashub.
Alizaliwa mwaka 489 katika mji wa Mazandarani ulioko kaskazini mwa Iran na kuaanza kutafuta elimu na maarifa katika kipindi cha ototoni. Bin Shahrashub alikuwa amekwishahifadhi Qur'ani nzima akiwa na umri wa miaka 8. Alipata ruhusa ya kunukuu Hadithi za Mtume (saw) kutoka maulamaa wakubwa wa zama hizo kama Zamakhshari, Muhammad Ghazali na Khatib Khorazmi na alikuwa hodari katika kutunga mashairi.
Mojawapo ya mashairi yake ya kuvutia ni lile alilotunga akitaja sifa na matukufu ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Shairi hilo linapatikana katika kitabu cha Manaqib Aal Abi Twalib.
Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika elimu za Hadithi na sayansi ya Qur'ani Tukufu. ***
Siku kama ya leo miaka 674 iliyopita Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi Mwislamu wa Misri alizaliwa huko Cairo nchini Misri.
Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lengo la kupata elimu ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba lifahamika kwa jina la Muhifadhi Mkubwa wa Hadithi.
Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaan al-Mizaan, Fat'hul-Bari fii Sharh Hadithul-Bukhari na al-Isabah fii Tamyizi Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria. ***
Siku kama ya leo miaka 376 iliyopita alifariki dunia René Descartes, mwanafalsafa na mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa.
Alizaliwa tarehe 31 Machi 1596 Miladia na baada ya masomo yake ya msingi alianza kusomea hisabati na tiba. Baadaye Descartes alibobea katika taaluma za hisabati na uhandisi na baadaye akianzisha utafiti katika uga wa falsafa.
Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo.
Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method. ***
Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita alifariki dunia Allamah Sheikh Muhammad Jawad Balaghi, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu.
Katika zama zake alikuwa mtaalamu wa elimu ya fiqhi, mwalimu na mwandishi mkubwa. Allamah Balaghi alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama zake kama vile Mirza Shirazi na kutokea kuwa mmoja wa walimu na waandishi wakubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al Balaghul-Mubin' kinachothibitisha uwepo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. *****
Tarehe 22 Bahman miaka 47 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote.
Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi.
Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme.
Wakati ilipotangazwa habari kwamba vifaru vya majeshi ya Shah vilikuwa njiani kuelekea Tehran kwa ajili ya kukandamiza harakati za mapinduzi zilizokuwa zinaelekea kileleni, wananchi wa miji mbalimbali walijitokeza na kupambana na majeshi hayo huku wakifunga njia na kuzuia misafara ya vifaru hivyo. Baadhi ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Shah waliuawa na wananchi katika mapambano hayo na kulilazimisha jeshi kutopendelea upande wowote.
Siku hiyo pia wananchi wanamapinduzi walitwaa Shirika la Redio na Televisheni la Iran kutoka kwenye udhibiti wa jeshi. Muda mfupi baadaye lilitolewa tangazo katika redio ya taifa likitangaza kwamba "Hii ni Sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu". Sauti hiyo ilitangaza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuporomoka utawala wa kidhalimu wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka 2500. ***
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita sawa na tarehe 11 Februari 1990, Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati ya kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa miaka 27.
Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 1963 kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.
Baada ya miaka kadhaa aliachiliwa huru kutokana na msimamo wake thabiti akiwa jela, mapambano ya wananchi wa nchi hiyo pamoja na mashinikizo yaliyotokana na fikra za waliowengi duniani. ***