Alkhamisi, tarehe 5 Disemba, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 03 Jumadithani 1446 Hijria sawa na Disemba 5 mwaka 2024.
Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Jamadi Thani sawa na 05 Disemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya wahyi na ufunuo.
Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as).

Siku kama ya leo miaka 787 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na msomi wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo. Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia.
Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alifundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi. Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi; na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw).
Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, aliaga dunia Alexandre Dumas mwandishi mtajika wa Kifaransa.
Mwandishi huyo ambaye ni mashuhuri pia kwa jina la Dumas Baba baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa katika ofisi moja ya kiwanda kama katibu kutokana na kuwa na hati nzuri.

Katika siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, Iran ilijiunga na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu.
Jitihada za awali za Iran kutaka kujiunga na shirika hilo zinarejea nyuma katika kipindi cha utawala wa Mfalme Nassereddin Shah Qajar.
Katika kipindi cha utawala wake, Disemba 1874 Iran iliukubali mkataba uliopasishwa Geneva Uswisi, lakini licha ya kupita miaka kumi tangu isaini mkataba huo, utawala wake haukuchukua hatua yoyote ile ya kuasisi taasisi au jumuiya ambayo itatekeleza hati ya mkataba huo hapa Iran.

Miaka 123 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Walt Disney shakhsia mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto.
Disney alizaliwa katika mji wa Chicago huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art).
Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni. Miongoni mwa kazi muhimu za Walt Disney ni Snow White, The Seven Dwarfs, Polar Bears.

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita alifariki dunia shujaa wa mapambano ya ukombozi na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela akiwa na umri wa miaka 95.
Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alitumia zaidi ya nusu ya umri wake akipambana na utawala wa kibaguzi nchini kwake. Utawala wa wazungu wabaguzi ulimfunga jela kwa kipindi cha miaka 27 hadi mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipofutwa mwaka 1990.
Mwaka 1994 wananchi wa Afrika Kusini walimchagua Nelson Mandela kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo. Baada ya kushika hatamu za uongozi, Mandela aliamiliana vyema na watala wa zamani wa mfumo wa ubaguzi wa rangi na hata wale waliomfunga jela na kumtesa. Mwenendo huo wa kusamehe ulizidisha umashuhuri na kupendwa shujaa huyo, na mwaka 1993 alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel.
Kitabu mashuhuri zaidi cha shujaa huyo wa Afrika ni kile chenye kumbukumbu zake alichokipa jina la: "Njia Ndefu ya Kuelekea kwenye Uhuru".

Na leo, Disemba 5, ni Siku ya Kimataifa ya Wahisani ambao hujitolea kwa hali na mali kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine. Kutenda wema na kufanya hisani ni suala ambalo halihusu, dini, taifa, wala kaumu makhsusi. Hata hivyo Uislamu ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu, umehimiza zaidi kutenda wema na hisani na kuwataja wahisani na watenda wema kwamba ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Sehemu ya Aya ya 195 ya Suratul Baqara inasema: Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wahisani.
