Magaidi 6 watiwa mbaroni kwa kujaribu kumuua rais wa Venezuela
(last modified Mon, 06 Aug 2018 08:04:16 GMT )
Aug 06, 2018 08:04 UTC
  • Magaidi 6 watiwa mbaroni kwa kujaribu kumuua rais wa Venezuela

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela jana usiku alitoa tamko na kutangaza habari ya kutiwa mbaroni magaidi 6 waliohusika na jaribio lililoshindwa la kutaka kumuu Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo.

Nestor Reverol, waziri wa mambo ya ndani wa Venezuela amesema katika tamko lake hilo kuwa mmoja wa magaidi hao sita alihusika katika shambulio la mwaka 2017 dhidi ya kambi ya kijeshi iliyoko katika mji wa Valencia, makao makuu ya jimbo la Carabobo huko Venezuela. Magaidi wengine kati ya hao walishiriki katika uasi na machafuko yaliyoikumba Venezuel mwaka 2014.

Walinzi wakimuhami Rais Nicolas Maduro wa Venezuela baada ya jaribio la kutaka kumuua

 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuel ameongeza kuwa, jeshi la polisi linaendelea na msako na hadi sasa limeshagundua magari na mikanda kadhaa ya filamu inayohusiana na jaribio lililoshindwa la kutaka kumuua rais wa nchi hiyo.

Mapema jana Jumapili, kulitokea jaribio la kutaka kumuua Rais Nicolas Maduro wa Venezuela wakati alipokuwa anatoa hotuba katika sherehe za kijeshi huko Caracas, mji mkuu wa nchi hiyo.

Baada ya tukio hilo, Jorge Jesús Rodríguez, waziri wa usalama wa taifa wa Venezuela alisema kuwa, ndege isiyo na rubani yaani drone iliruka karibu na eneo alilokuwa anahutubia Rais Maduro ikiwa na mada za miripuko na kuripuka katika eneo hilo. Hata hivyo Maduro amesalimika katika jaribio hilo, ingawa wanajeshi 7 wamejeruhiwa. 

Rais Maduro amezishutumu Marekani na Columbia kwa kuhusika na jaribio hilo la kigaidi la kutaka kummalizia maisha.

Tags