Venezuela: Faili la kutaka kumuu Rais Maduro litashughulikiwa kimataifa
(last modified Sat, 11 Aug 2018 04:04:39 GMT )
Aug 11, 2018 04:04 UTC
  • Venezuela: Faili la kutaka kumuu Rais Maduro litashughulikiwa kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo inakusudia kuliwasilisha faili la jaribio la kutaka kumuu Rais Nicolás Maduro wa nchi hiyo katika ngazi ya kimataifa.

Jorge Arreaza ameyasema hayo wakati akiashiria njama iliyoshindwa ya hivi karibuni ya kutaka kumuua Rais Maduro na kusema kuwa, taarifa za upelelezi wa faili hilo la kigaidi zitawasilishwa katika nyuga za kimataifa. Kadhalika alipokutana na wanadiplomasia wa Colombia katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Caracas, Arreaza amewasilisha rasmi ombi la serikali ya Venezuela kwa balozi wa taifa hilo kufikisha ujumbe kwa nchi yake wa kuwakabidhi washukiwa wanaoaminiwa na Venezuela kuwa walihusika na hujuma hiyo.

Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela

Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela imetangaza kwamba, Caracas pia imeitaka serikali ya Marekani kuikabidhi washukiwa wa shambulizi hilo la hivi karibuni. Awali Wizara ya Mambo ya Ndani ya Venezuela ilitangaza kwamba, watu wanaodhaniwa kwamba waliratibu shambulizi hilo ni 25. 

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela alinusurika jaribio la mauaji lililofanywa na kitu kinachoaminika kuwa ni ndege isiyo na rubani (drone). Shambulizi hilo lilifanyika wakati Rais Maduro alipokuwa akihutubia katika kambi ya jeshi usiku wa kuamkia tarehe tano ya mwezi huu. Baada ya kunusurika jaribio hilo, Maduro alisema kuwa Marekani na Colombia ndizo zilizofanya jaribio la kutaka kumuua.

Tags