China: Hatutasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani kuihusu Iran
Mkuu wa Shirikisho la Sekta ya Mafuta na Bidhaa za Kemikali nchini China amesema kuwa, Beijing haina nia ya kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani kwa ajili ya kutekeleza vikwazo vya upande mmoja vya Washington dhidi ya Iran.
Andrey Yu amesema kuwa, mashirika ya China hayajasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani kama ambavyo Beijing haivipi umuhimu wowote vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Aidha amefafanua kuwa, Iran ni moja ya washirika wakubwa wa kibiashara wa China na Beijing itaendelea kununua mafuta ya Iran sambamba na kupuuza mashinikizo na vitisho vya Marekani. Mkuu wa Shirikisho la Sekta ya Mafuta na Bidhaa za Kemikali nchini China sambamba na kukosoa ubeberu wa Marekani juu ya vyanzo vya mafuta na gesi katika maeneo tofauti ya dunia hususan eneo la Mashariki ya Kati amesema kuwa, sekta zinazohusiana na nishati ya fosili na biashara, hazitakiwi kuwa chini ya ushawishi wa Marekani.
Awali Shirika la Taifa la Mafuta nchini China lilitangaza kwamba, iwapo washirika wengine watalazimika kuacha kununua nishati ya Iran kutokana na mashinikizo ya Marekani, basi shirika hilo lipo tayari kuchukua nafasi yao. Serikali ya Marekani imekusudia kuzuia mauzo ya mafuta ya Iran kufikia sifuri kuanzia tarehe nne Novemba. Sambamba na hayo Marekani imezitaka nchi zote za dunia kushiriki vikwazo vyake vya kiuchumi dhidi ya Iran kwa kuacha kununua mafuta ya Iran, suala ambalo nchi nyingi zimetangaza bayana kwamba hazitofungamana na matakwa hayo ya Marekani.