Italia yakata misaada yake kwa Umoja wa Ulaya (EU)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia ametangaza kuwa nchi hiyo imekata misaada yake kwa Umoja wa Ulaya kufuatia kuendelea mivutano kati ya umoja huo na Italia kuhusu suala la wahajiri waliokwama katika meli ya gadi ya pwani ya Italia kwa jina la Diciotti (Dichuti).
Enzo Muavero Milanesi Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amezikosoa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala la wahajiri na kuzitaka ziwajibike zaidi katika uwanja huo kufuatia kuendelea hali ya mvutano kuhusu meli hiyo ya Diciotti iliyobeba wahajiri. Milanesi ameashiria kukatwa misaada ya nchi yake kwa Umoja wa Ulaya na wakati huo huo akasema anataraji kuwa Italia itafikia mapatano ya pamoja na nchi nyingine za Ulaya kuhusu kadhia hii ya wahajiri waliokwama.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesisitiza kuwa Roma inakubali kuwa watu waliopo baharini na katika hali ngumu wanapasa kuokolewa hata hivyo akasema Umoja wa Ulaya unapasa pia kushughulikia tatizo la wahajiri iwapo unataka kudumisha hadhi ya umoja huo. Hatua ya kukwama katika bandari ya Katania kusini mwa Italia meli ya Diciotti (Dichuti) yenye wahajiri 150 imeibua mvutano kati ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya. Meli hiyo ilikwama tangu Jumatatu iliyopita huku wahajiri wakinyimwa kibali cha kutoka katika meli hiyo.