Njama za kuingilia kijeshi masuala ya ndani ya Venezuela
(last modified Sun, 16 Sep 2018 11:04:37 GMT )
Sep 16, 2018 11:04 UTC
  • Njama za kuingilia kijeshi masuala ya ndani ya Venezuela

Luis Almagro, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Amerika ametoa matamshi ya vitisho dhidi ya Venezuela na kusema kuwa, chaguo la kijeshi kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela halipasi kupuuzwa.

Almagro amemtuhumu Rais Maduro kuwa muhusika mkuu wa kushadidi mgogoro wa kiuchumi, kibinaadamu na kiuhajiri nchini humo. Matamshi na radiamali ya jumuiya hiyo ya nchi za Amerika yanatolewa katika hali ambayo Venezuela imetangaza rasmi kwamba, itashirikiana kikamilifu na Umoja wa Mataifa katika nyanja zote hususan kuhusiana na suala la haki za binaadamu. Pamoja na hayo, matamshi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Amerika yanaonyesha kuwa taasisi hiyo ni chombo kilicho chini ya udhibiti wa Marekani na inayotekeleza siasa za madola ya kibeberu. Tunaweza kusema kuwa, hivi sasa serikali ya Marekani iko mbioni kuhuisha siasa za mauaji ya kuvizia na mapinduzi ya kijeshi dhidi ya nchi za Amerika ya Latini na baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati.

Luis Almagro, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Amerika ambaye anatajwa kuwa kibaraka wa Marekani

Katika uwanja huo, viongozi wa sasa wa serikali ya Washington wamekuwa na vikao vya siri na viongozi wa upinzani nchini Venezuela, kwa lengo la kuiondoa kwa nguvu madarakani serikali ya sasa ya Caracas. Katika hali ambayo, Rais Nicolás Maduro alishinda kidemokrasia uchaguzi huru uliofanyika hivi karibuni na kuwa rais halali wa Venezuela, Marekani ambayo imekuwa ikijidai kuwa muungaji mkono wa demokrasia na haki za binaadamu duniani, inatekeleza njama za uingiliaji ndani ya nchi hiyo. Kwa hakika hatua na njama hizo za wazi kwa ajili ya kufanya mapinduzi ya kijeshi na mauaji dhidi ya rais halali wa nchi iliyo huru, ni kinyume na misingi yote ya sheria za kimataifa. Hata hivyo Washington na kwa kuzitumia taasisi vibaraka kama vile Jumuiya ya Nchi za Amerika, imekuwa ikiziwekea mashinikizo nchi za eneo la Amerika ya Latini ili kwa njia hiyo iweze kupanua wigo wa siasa zake za kikoloni ndani ya eneo hilo. Ni wazi kuwa Jumuiya ya Nchi za Amerika pamoja na katibu mkuu wake, wanatumiwa na Marekani kutekeleza siasa za mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Venezuela. Hii ni kusema kuwa, Washington na Luis Almagro, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo hawafurahishwi na uwepo wa serikali ya mrengo wa kushoto nchini Venezuela na ni kwa msingi huo ndipo wakaanzisha njama za kutaka kudhoofisha na hatimaye kuing'oa kabisa madarakani serikali ya Rais Nicolás Maduro wa nchi hiyo. Kuna nyaraka nyingi zinazothibitisha uwepo wa uingiliaji wa Marekani nchini Venezuela ambapo aghlabu yazo zimetangazwa na hata vyombo vya habari vya ndani ya Marekani yenyewe, kiasi kwamba gazeti la New York Times limefichua mapinduzi matatu ya kijeshi yaliyopangwa kutekelezwa nchini Venezuela kati ya mwaka 2017 na 2018 kwa msaada wa serikali ya Marekani.

Rais Nicolás Maduro, anayekabiliwa na njama za kila uchao za Marekani

Hata hivyo njama zote hizo ziliishia kufeli. Gazeti la New York Times limefafanua kuwa, historia mbaya ya uingiliaji wa Marekani bado inaendelea kushuhudiwa hadi sasa katika nchi za Amerika ya Latini. Kuhusiana na suala hilo, Rideran Roet, mkuu wa kitengo cha utafiti wa masuala ya Amerika ya Latini katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins cha Maryland nchini Marekani anasema: "Hatua za uhasama za Marekani zinaifanya Washington kuchukuliwa kuwa inayotumia mabavu, jambo ambalo linahesabiwa kuwa ni zawadi kwa waungaji mkono wa rais wa zamani wa Venezuela Hugo Chávez na viongozi wengine wa mrengo wa kushoto katika eneo la Amerika ya Latini, ambapo hatimaye siasa hizo hupelekea mirengo ya kushoto kuibuka na ushindi." Mwisho wa kunukuu. Alaakullihal, njama za Marekani kama vile mapinduzi ya kijeshi na mauaji ya kigaidi, zinaonyesha kufeli wapangaji wake wenye lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Venezuela na hakuna shaka kwamba hatua hiyo itakuwa na matokeo kinyume na wanavyotarajia. Kudhihiri nguvu mpya katika eneo la Amerika ya Latini kunaufanya ubeberu wa Marekani kuendelea kusambaratika ambapo nchi huru ndizo zitaibuka kuwa washindi katika vita hivyo.

Tags