Rais Tayyip Erdoğan: Marekani inajaribu kuua kigaidi uchumi wa Uturuki
Kwa mara nyingine Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesisitiza kwamba, Marekani iko nyuma ya vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa dhidi ya nchi yake.
Rais Erdoğan ameyasema hayo akiwahutubia wafuasi wa chama chake ambapo ametaka kuimarishwa nafasi ya fedha ya kitaifa ya Lira ya nchi hiyo katika mabadilishano na nchi nyingine. "Tunakabiliwa na shambulizi la uchumi wa nchi yetu, na kuporomoka thamani ya sarafu ya Lira ni njama za adui kwa ajili ya kuua kigaidi uchumi wa Uturuki." Amesema Rais Erdoğan. Serikali ya Ankara inafanya juhudi kwa ajili ya kurejesha uthabiti wa sarafu yake ya Lira ambapo tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa fedha hiyo imepoteza karibu asilimia 40 ya thamani yake mkabala wa Dola ya Kimarekani.
Katika uwanja huo Rais Recep Tayyip Erdoğan amewataka raia wa Uturuki kutoa akiba zao za fedha za kigeni na kuzibadili kwa fedha ya Lira, sambamba na kuiamini sarafu hiyo. Uhusiano wa Uturuki na Marekani ulihaibika tangu kujiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 2016 na baada ya kutiwa mbaroni padri wa Kimarekani Andrew Brunson ambaye anatuhumiwa kufanya ujasusi na kushirikiana na magaidi. Kufuatia hatua hiyo serikali ya Marekani iliwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Rais Erdoğan. Hii ni katika hali ambayo padri huyo amehukumiwa kifungo cha miaka 35 na serikali ya Uturuki.