UNICEF: Katika kila sekunde tano, mtoto mmoja hufariki dunia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48221-unicef_katika_kila_sekunde_tano_mtoto_mmoja_hufariki_dunia
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef umesema watoto milioni 6.3 waliaga dunia kabla ya kufikisha miaka 15 mwaka jana 2017, huku nusu ya vifo hivyo vikiripotiwa katika eneo la chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 18, 2018 02:55 UTC
  • UNICEF: Katika kila sekunde tano, mtoto mmoja hufariki dunia

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef umesema watoto milioni 6.3 waliaga dunia kabla ya kufikisha miaka 15 mwaka jana 2017, huku nusu ya vifo hivyo vikiripotiwa katika eneo la chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika.

Laurence Chandy, mtalaamu wa Unicef amesema mtoto mmoja hupoteza maisha katika kila sekunde tano, aghalabu ya vifo hivyo vikiripotiwa kutokana na ukosefu wa maji safi ya kunywa, lishe bora, huduma za msingi za afya na vyoo.

Amesema kati ya vifo milioni 6.3 vya watoto hao, milioni 5.4 viliwakumba watoto wadogo ambao hawajafikisha umri wa miaka mitano.

Afisa huyo wa Unicef ametahadharisha kuwa, iwapo hatua za dharura na makusudi hazitachukuliwa, yumkini watoto wadogo milioni 56 wenye chini ya miaka mitano wakapoteza maisha, kati ya sasa na mwaka 2030. Amesema asilimia 50 ya vifo hivyo hutokea wakati wa kuzaliwa watoto hao.

Mtoto mwenye utapiamlo nchini Yemen

Kwa mujibu wa takwimu hizo mpya zilizotolewa leo Jumanne na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa, watoto milioni 2.5 waliaga dunia kabla ya kumaliza mwezi mmoja wa uhai wao mwaka jana 2017.

Ripoti ya Unicef imesisitiza kwamba, mtoto anayezaliwa katika nchi za chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika na kusini mwa Asia yuko katika hatari mara tisa ya kupoteza maisha kabla ya kumaliza mwezi mmoja, kuliko watoto wanaozaliwa katika nchi zilizostawi kiuchumi.