Marekani: Tupo tayari kuanza upya mazungumza na Korea Kaskazini
(last modified Thu, 20 Sep 2018 15:08:37 GMT )
Sep 20, 2018 15:08 UTC
  • Marekani: Tupo tayari kuanza upya mazungumza na Korea Kaskazini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa, nchi yake imejiandaa kuanza haraka mazungumzo ya kutokomeza silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na kwamba mazungumzo hayo yatakamilika ifikapo mwezi Januari 2021.

Mike Pompeo sambamba na kusema hayo, amewataka viongozi wa Korea Kaskazini kukutana haraka na Steve Biegun, mjumbe maalumu wa White House katika masuala ya nchi hiyo ya Asia, huko mjini Vienna, Austria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameashiria matamshi ya Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini juu ya kuharibu kituo cha nyuklia cha Tongchang-ri na kusema kuwa, mwenendo wa kuharibiwa eneo hilo ni lazima ufanyike chini ya uangalizi kamili wa wataalamu wa kimataifa na Marekani, kwa kuwa hatua hiyo ni njia ya kuelekea kutokomezwa kikamilifu silaha za Korea Kaskazini.

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini

Kufuatia mvutano wa kimaneno wa mwaka mzima kati ya Washington na Pyongyang, Rais Donald Trump wa Marekani na Kim Jong-un walikutana nchini Singapore hapo tarehe 12 Juni mwaka huu ambapo baada ya mazungumzo baina yao walitiliana saini makubaliano kadhaa yakiwemo ya kuangamizwa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini huku Marekani ikitakiwa kuidhaminia Pyongyang usalama wake. Hata hivyo misimamo hasi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuizidishia mashinikizo na vikwazo, ilipelekea kusimama utekelezaji wa makubaliano hayo.

Katika uwanja huo, Trump alimzuia Mike Pompeo kufanya safari mjini Pyongyang sambamba na kudai kuwa hakuona maslahi katika kuendeleza mazungumzo na Korea Kaskazini. Serikali ya Pyongyang inaituhumu Marekani kuwa imekiuka makubaliano ya Singapore.

Tags