Oct 06, 2018 03:48 UTC
  • Hofu ya UN juu ya kufukuzwa India wakimbizi wa Rohingya

Umoja wa Mataifa umeonesha kutiwa wasiwasi mkubwa na hatua ya India ya kuwafukuza wakimbizi Waislamu wa Rohingya na kuwarejesha nchini Myanmar.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Geneva jana Ijumaa, Andrej Mahecic, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR alisema, "Shirika hili linatafuta ufafanuzi kutoka serikali ya India kuhusu kuwafukuza wakimbizi hao na kuyaweka maisha yao hatarini. Tunataka kujua mbona hawakupewa fursa ya kuanzisha mchakato wa kupewa hifadhi? Kuwafukuza kwa nguvu ni ukiukaji wa sheria za kimataifa."

Siku ya Alkhamisi, serikali ya New Delhi iliwafukuza na kuwarejesha nchini Myanmar, wakimbizi saba wa Rohingya, ambao wamekuwa wakizuiliwa na vyombo vya usalama nchini humo, kwa madai ya kuingia nchini humo kinyume cha sheria.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya India sambamba na kudai kuwa uwepo wa wakimbizi hao Waislamu nchini India si halali, imezitaka tawala za majimbo yote ya nchi hiyo kutoa taarifa za wakimbizi hao kwa ajili ya kuwaondoa India na kuwarejesha nchini kwao Myanmar. 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, wakimbizi Waislamu wa Rohingya nchini India ni elfu 40.

Jinai kubwa za jeshi la serikali ya Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha magaidi wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine, la magharibi mwa nchi hiyo zilianza tarehe 25 Agosti mwaka jana na zilipelekea maelfu ya watu kuuawa.

Akthari ya nchi za dunia zimelaani vikali mauaji hayo ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya na kuyataka madola ya Magharibi kuchukua hatua kali dhidi ya serikali ya Myanmar ingawa hadi hvi sasa tawala hizo hazijachukua hatua yoyote ya maana.

Tags