Warohingya: Bora tuuliwe India kuliko kurejeshwa Myanmar
Wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaoishi kambini nchini India wamesema afadhali wauawe wakiwa ndani ya nchi hiyo badala ya kurejeshwa nchini kwao Myanmar.
Wakimbizi hao wanaoshi katika kambi zilizoko katika mtaa wa Kalindi Kunj viungani mwa mji mkuu New Delhi, wameiambia kanali ya televisheni ya al-Jazeera kuwa, hawako tayari kurejeshwa kwa nguvu nchini Mynamar na bora wauawe wakiwa nchini India kulikoni kurejeshwa nchini kwao.
Mapema mwezi huu, serikali ya New Delhi iliwafukuza na kuwarejesha nchini Myanmar, wakimbizi saba wa Rohingya, ambao wamekuwa wakizuiliwa na vyombo vya usalama nchini humo, kwa madai ya kuingia nchini humo kinyume cha sheria.
India inatekeleza mpango huo wa kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi Waislamu wa Rohingya nchini Mynamra katika hali ambayo, wiki iliyopita, ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR ilisisitiza kuwa Waislamu Warohingya wangali wanaishi kwa hofu na hawana imani yoyote kuhusu usalama wao mbali na kunyimwa hata ruhusa ya kutembea kwa uhuru katika eneo wanaloishi la mkoa wa Rakhine.
Msemaji wa UNHCR amesema, Waislamu hao wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku kutokana na kutokuwepo usalama na vizuizi vya kutembea walivyowekewa, na kwamba serikali ya nchi hiyo haijatayarisha mazingira yoyote ya kuwawezesha Waislamu Warohingya kurejea kwenye maisha yao ya kawaida.