UN yalaani jinai mpya za Wazayuni Palestina
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuwaua watoto wa Palestina hakikubaliki kabisa.
Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya umoja huo huko New York Marekani kwamba, Katibu Mkuu wa UN António Guterres, amesikitishwa sana na kitendo cha Israel cha kuwaua shahidi watoto watatu wa Palestina huko Ghaza, na ametaka kuchukuliwa hatua za makusudi za kulindwa roho za watoto wa Kipalestina.
Wakati huo huo Nickolay Mladenov, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya amani ya Mashariki ya Kati ametuma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuelezea kusikitishwa sana na mauaji ya watoto hao watatu wa Palestina yaliyofanywa na wanajeshi katili wa Israel. Amesema, haipasi kuwatia hatarini watoto wadogo.
Kabla ya hapo pia, Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO kilikuwa kimeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuuchukulia hatua utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kuwaua shahidi watoto watatu wa Kipalestina huko Ghaza.
Jumapili usiku, wanajeshi makatili wa Israel walifanya mashambulizi katika eneo la Deir al Bahal, katikati ya Ukanda wa Ghaza na kuwaua shahidi watoto watatu wa Kipalestina.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya jinai za kila namna dhidi ya Wapalestina kwa kutumia vibaya udhaifu wa Umoja wa Mataifa na dharau ya nchi zinazodai kutetea haki za binadamu ulimwenguni. Takwimu zinaonesha kuwa, tangu mwaka 1967 hadi 2017, utawala wa Kizayuni wa Israel umeua zaidi ya Wapalestina 42 elfu na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine.