Zaidi ya watu 2000 wamepoteza maisha 2018 wakijaribu kuvuka Mediterania
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49354-zaidi_ya_watu_2000_wamepoteza_maisha_2018_wakijaribu_kuvuka_mediterania
Idadi ya watu waliopoteza maisha wakivuka bahari ya Mediteranea mwaka huu wakitafuta hifadhi Ulaya imepindukia 2000 baaada ya maiti 17 kupatikana kwenye ufukwe wa Hispania wiki hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2018 13:18 UTC
  • Zaidi ya watu 2000 wamepoteza maisha 2018 wakijaribu kuvuka Mediterania

Idadi ya watu waliopoteza maisha wakivuka bahari ya Mediteranea mwaka huu wakitafuta hifadhi Ulaya imepindukia 2000 baaada ya maiti 17 kupatikana kwenye ufukwe wa Hispania wiki hii.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema hayo katika taarifa iliyotolewa mjini Geneva Uswisi ikiangazia idadi ya watu waliopoteza maisha mwaka huu pekee na wahamiaji na wakimbizi walioweza kufika barani Ulaya.

Idadi kubwa ya vifo yaani takribani nusu ya vifo vyote vilivyoripotiwa vilitokea katika maeneo ya kuingia nchini Italia ingawa wengi waliofanikiwa kuvuka waliiingia nchini Uhispania. Zaidi ya watu 48,000 wameingia Uhispania kwa njia ya bahari, ikilinganishwa na takribani watu 22,000 walioingia Italia na 27,000 walioingia Ugiriki.

UNHCR imekuwa ikitaka zichukuliwe hatua za kulitatua suala hili la wahamiaji kupoteza maisha katika harakati za kuzihama nchi zao na kutafuta makazi katika nchi za Ulaya kupitia njia ya  bahari ya Mediterania ambayo kwa miaka kadhaa imekuwa njia ya hatari zaidi kwa wakimbizi na wahamiaji.

Meli ya wahajiri ikizama 

Takribani watafuta hifadhi 100,000 wamefika barani Ulaya hadi sasa mwaka huu, ingawa idadi ya vifo ni kubwa.

UNHCR inasisitiza kuwa watu wote wanaookolewa katika eneo la maji la kimataifa yaani maili 12 kutoka eneo la maji yaliyoko katika himaya ya Libya, hawatakiwi kurejeshwa nchini Libya ambako hali si shwari.

Shirika hilo pia linarudia tena wito wake kwa jumuiya ya kimataifa kutafuta visababishi vinavyowalazimisha watu kuhama na kupitia njia zile zile za hatari.