Wanaharakati 3000 wataka kususiwa mkutano dhidi ya Iran huko Poland
Wanaharakati 3000 wanaopinga vita huko Marekani na katika nchi nyingine duniani wametia saini hati inayozitaka nchi za Ulaya kususia mkutano wa kuipiga vita Iran uliopangwa kufanyika nchini Poland.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo kudai kuwa, zaidi ya nchi 70 zitashiriki katika mkutano huo unaotayarishwa na serikali ya Washington.
Baada ya madai hayo, wanaharakati wa Marekani na nchi nyingine wanaopinga sera za vita za Marekani wameanzisha kampeni katika wavuti ya jumuiya isiyo ya serikali ya Codepink wakizitaka nchi za Ulaya zisusie vita vya Mike Pompeo dhidi ya Iran.
Kampeni hiyo ambayo hadi sasa inawashirikisha wanaharakati karibu elfu tatu chini ya kaulimbiu ya "Amani na Iran", inazitaka nchi za Ulaya kususia mkutano uliodhidi ya Iran wa Marekani uliopangwa kufanyika tarehe 13 na 14 Februari nchini Poland.
Kampeni hiyo inasisitiza kuwa, lengo la mkutano huo ni kutayarisha mazingira ya kuanzisha vita visivyo vya lazima dhidi ya Iran na kwamba badala ya kukabiliana na Iran kuna udharura wa kuishinikiza zaidi Marekiani ili irejee katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kufuta vikwazo haribifu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Wanaharakati hao wanasisitiza kuwa, baada ya kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Donald Trump amezidisha uhasama dhidi ya Iran na kuhatarisha zaidi usalama wa eneo la Mashariki ya Kati.
Wanaharakati hao wamezitaka nchi za Ulaya kuitisha mkutano mbadala wa kujadili masuala ya Mashariki ya Kati utakaozishiriki nchi za eneo hilo ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.