Umoja wa Afrika watangaza kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro wa Venezuela
(last modified Thu, 31 Jan 2019 04:43:03 GMT )
Jan 31, 2019 04:43 UTC
  • Umoja wa Afrika watangaza kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro wa Venezuela

Wizara ya Mambo ya Nje ya Venezuela imetangaza kwamba Umoja wa Afrika umesisitiza kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro wa nchi hiyo.

Wizara hiyo imenukuu habari hiyo kutoka kwa Modesto Leite balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia baada ya balozi huyo kufanya mazungumzo na Thomas Kwesi Quartey, Naibu Mwenyekiti wa Umoja huo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kwesi ametangaza uungaji mkono wa Umoja wa Afrika kwa raia na serikali ya Rais Nicolás Maduro kama ambavyo amemtaja kuwa rais halali wa nchi hiyo. Kabla ya hapo pia Jerry Matjila, Mwakilishi wa Kudumu wa Afrika Kusini katika Umoja wa Mataifa alisisitiza kwamba, nchi yake inamuunga mkono Rais Maduro na kwamba itaendelea na msimamo wake huo. 

Njama chafu za Trump za kutaka kufanya mapinduzi dhidi ya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela

Katika hatua nyingine Rais Nicolás Maduro amelitaka jeshi kuungana kwa ajili ya kuzuia uasi ulioitishwa na Rais Donald Trump wa Marekani pamoja na Juan Guaidó kiongozi wa wapinzani aliyejitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo. Rais Maduro ametoa mwito huo baada ya kiongozi huyo wa upinzani kutaka kuratibu maandamano mapya nchini humo. Licha ya Marekani, utawala haramu wa Israel na baadhi ya nchi za Ulaya na eneo la Amerika ya Latini kutangaza kumuunga mkono Juan Guaidó, lakini nchi za Russia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, China, Uturuki, Mexico, Cuba, Afrika Kusini na nchi nyingine nyingi za dunia zimetangaza kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro ambaye alichaguliwa mwaka jana na wananchi kuwa rais halali wa Venezuela.

 

Tags