Kushadidishwa mashinikizo dhidi ya Venezuela
(last modified Sat, 02 Feb 2019 02:44:17 GMT )
Feb 02, 2019 02:44 UTC
  • Kushadidishwa mashinikizo dhidi ya Venezuela

Kufuatia kudhihiri mgogoro wa kisiasa wa Venezuela, nchi za Magharibi zimekuwa zikifanya juhudi kubwa za kufikia malengo yao katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini iliyo na utajiri mkubwa wa mafuta.

Baada ya Juan Guaido, spika aliyefutwa kazi wa bunge la Venezuela, kujitangaza tarehe 23 Januari kuwa rais wa muda wa nchi hiyo, nchi za Magharibi zimetangaza uungaji mkono wao mkubwa kwake. Mtu wa kwanza kutangaza uungaji mkono huo, alikuwa ni rais Donald Trump wa Marekani ambaye kupitia taarifa alimtambua rasmi Guaido kuwa rais wa Venezuela, na kusema kuwa atampa kila aia ya msaada wa kiuchumi na kidiplomasia kwa ajili ya kuimarisha nchini humo kile alichokitaja kuwa demokrasia. Mansur Muadhami, mtaalamu wa Masuala ya Amerika ya Latini anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba Marekani, washirika wake wa Ulaya na baadhi ya nchi za Amerika ya Latini zimeanzisha mfano mbaya na hatari, kwa kumtamua rasmi mtu aliyejitangaza mwenyewe kuwa rais wa muda wa nchi inayojitawala. Hivi sasa Ulaya imeingia rasmi kwenye mchezo huo mchafu kufuatia hataua ya uingiliaji ya hivi karibuni ya Bunge la Ulaya ambalo limepitisha mswada wa kumtambua rasmi kiongozi huyo wa upinzani wa Venezuela kuwa rais wa nchi hiyo, na kuzitaka nchi wanachama pia kumtambua Guaido kuwa rais wa nchi hiyo.

Juan Guaido, kibaraka wa nchi za Magharibi nchini Venezuela

Tokea wiki iliyopita ambapo Guaido alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela, nchi za Ulaya moja baada ya nyingine zimetangaza rasmi uungaji mkono wao kwa kiongozi huyo wa upinzani kwa kisingizio cha kutetea demokrasia. Hatua hiyo ya uingiliaji ambayo inatekelezwa kinyume kabisa na sheria za kimataifa, na ambao ni mfano wa wazi wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, inatekelezwa kwa madhumuni ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Nicolas Maduro, rais halali wa Venezuela ili kumlazimisha ajiengue madarakani. Uingiliaji rasmi wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya ndani ya Venezuela na vilevile mapinduzi ya kisiasa ya Marekani yanatekelezwa katika hali ambayo Rais Maduro alishinda kwa asilimia 68 ya kura zilizopigwa na wananchi katika uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika mwaka uliopita, na hivyo kupewa fursa na wananchi ya kuhudumia tena nafasi hiyo kwa kipindi cha pili. Katika upande wa pili, Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa wapinzani wa Venezuela imekuwa ikizidisha mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya serikali ya mrengo wa kushoto ya Maduro kwa kuiwekea kila aina ya vikwazo,  kuzuia fedha zake na kuzishaiwshi nchi nyingine zisifanye biashara nayo. Katika uwanja huo Marekani imeionya Uturuki dhidi ya kukiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela.

Rais Maduro aliye na uungaji mkono mkubwa wa wananchi na jeshi

Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Marekani alisema Alkhamisi kwamba Washington inafuatilia kwa karibu biashara kati ya Uturuki na washirika wa Marekani katika shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO na Venezuela, na kwamba itakapobainika kwamba Ankara inakiuka vikwazo hivyo vya Marekani, hatua inayofaa itachukuliwa. Hii ni katika hali ambayo Uturuki na nchi nyingine muhimu kama Russia, China na Iran zinamuunga mkono Maduro na serikali yake na kukemea vikali hatua za uingiliaji za nchi za Magharibi na Hasa Marekani katika mambo ya ndani ya Venezuela. Hatua za nchi hizo zinaonyesha wazi kwamba zinataka kutumia mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi na hata za kijeshi kumng'oa madarakani Rais Nicolas Maduro ambaye kufikia sasa amekuwa akitekeleza siasa huru zinazopingana na Marekani, na kumuweka mahala pake rais kibaraka atakayefuata na kutekeleza siasa zinazolinda maslahi ya nchi za Magharibi nchini humo.

Tags