Kulegeza msimamo Marekani kuhusu vitisho vyake vya kijeshi dhidi ya Venezuela
(last modified Sun, 03 Feb 2019 01:27:06 GMT )
Feb 03, 2019 01:27 UTC
  • Kulegeza msimamo Marekani kuhusu vitisho vyake vya kijeshi dhidi ya Venezuela

Katika hali ambayo Washington na waitifaki wake wangali wanafuatilia mpango wao wa kuipindua serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela; kusimama kidete na kuwa macho Rais Nicolaus Madurowa nchi hiyo na kuungwa mkono kwake na wananchi, si tu kuwa kumefelisha njama za pande hizo za kutekeleza njama zao dhidi ya Maduro bali kumeipelekea Washington pia kulegeza msimamo katika baadhi ya siasa zake.

Hivi karibuni John  Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House alisema kwamba Marekani kwa sasaa haina nia ya kuchukua hatua ya kijeshi huko Venezuela. 

Akiashiria matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani aliyesema kuwa machaguo yote yapo mezani, Bolton amebainisha  lengo la Washington kuwa ni kuona  madaraka yanakabidhiwa kwa amani huko Venezuela. Bolton amebainisha hayo katika hali ambayo suala la Marekani la kutaka kuingilia kijeshi huko Venezuela limekabiliwa na radiamali kali kutoka pande tofauti. Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza namna Marekani  ilivyokiuka vigezo vyote vya kimataifa kuhusiana na Venezuela na kueleza kuwa: Moscow itatekeleza hatua yoyote itakayohitajika kwa ajili ya kuiunga mkono serikali halali ya Venezuela. 

Marekani na nchi waitifaki wake katika wiki za karibuni zimemuunga mkono Juan Guaido kiongozi wa wapinzani wa serikali ya Venezuela ambaye Januari 23 mwaka huu alitangaza kuwa rais wa nchi hiyo lengo likiwa ni kufanya mapinduzi ya kisiasa nchini humo. Kuyaondoa mapato ya mafuta mikononi mwa mrengo wa kushoto, kuiingiza madarakani serikali ya mrengo wa kulia inayoungwa mkono na Marekani na pia kudhoofisha mhimili wa mrengo wa kushoto huko Amerika ya Latini ni moja ya sababu zilizotoa msukumo kwa Marekani na waitifaki wake kutaka kumpindua madarakani Maduro. Kuhusiana na suala hilo, Washington inafanya kila linalowezekana ili kuiweka serikali ya Venezuela chini ya mashikinikizo. Pamoja na hayo lakini Washington imegonga mwamba hadi sasa kwa hatua zake za kutumia vikwazo na vitisho kama wenzo dhidi ya Venezuela. Maduro na serikali yake ya mrengo wa kushoto, licha ya kuwepo mivutano na mashinikizo makubwa, lakini wameweza kukabiliana na njama zote hizo za Washington na waitifaki wake wa ndani na nje ya nchi, kutokana na kuungwa mkono pakubwa na wananchi wa Venezuela na vile vile jeshi la nchi hiyo. Wananchi wa miji mbalimbali ya Venezuela siku kadhaa zilizopita walifanya maandamanao ya kutangaza kumuunga mkono Rais Maduro. Aidha wafanyakazi wa Wizara ya Mafuta ya nchi hiyo walifanya maandamano kuonyesha uungaji mkono wao kwa Rais huyo wa Venezuela.  

Juan Guaido, aliyekuwa spika wa bunge la Venezuela ambaye amejitangaza kuwa rais wa nchi 

Delsey Rodriguez Makamu wa rais wa Venezuela amesema mbele ya hadhara ya maandamano ya wafuasi wa maduro huko Caracas mji mkuu wa Venezuela kwamba: Sura zote zilizokuwa zimejificha sasa zimedhihirika wazi kuanzia kwa Rais Donald Trump wa Marekani, Makamu wake Mike Pence na John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa ikulu ya nchi hiyo (White House) kwa sababu watu hawa wote bila kuficha wametamka bayana kuwa kwa udi na uvumba wanayataka  mafuta ya Venezuela. Jibu letu kwa vitendo vya kupenda makuu na kujitanua vya Marekani ni hili: Wamarekani achaneni na mafuta yetu.

Delsey Rodriguez, Makamu wa Rais wa Venezuela 

Hatua zote hizi zimeilazimisha Washington na waitifaki wake kulegeza msimamo wao mbele ya mashinikizo ya fikra za waliowengi na matakwa ya watu wa Venezuela; khususan vitisho vyake vya kijeshi dhidi ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia hayo, aghalabu ya wanasiasa wametoa kipaumbele cha awali kwa mazungumzo na diplomasia wakisema kwamba njia za amani zitumike kuhitimisha mgogoro wa Venezuela. Kwa kadiri kwamba Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye pia ametangaza  kuwa yupo tayari  kuzipatia ufumbuzi hitilafu za nchi hiyo. Hata kama Washington na waitifaki wake wanafanya kila linalowezekana ili kufanikisha njama yao ya kuipinduia serikali nchini Venezuela lakini inaonekana kuwa siasa za uingiliaji za Washington na washirika wake nchini humo zimegonga mwamba. Wananchi wa Venezuela, majeshi na wafanyakazi wa sekta ya mafuta ya nchi hiyo wangali wanaonyesha uungaji mkono na utiifu wao kwa Rais Maduro na thamani zilizo dhidi ya ubepari, huku nchi nyingi duniani pia zikiunga mkono mapambano ya Wavenezuela dhidi ya uistikbari. Hatua zote hizo na mashinikizo ya fikra za waliowengi yameilazimisha Marekani kulegeza msimamo na kuachana na vitisho vyake vya kutaka kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya serikali halali iliyochaguliwa na wananchi wa Venezuela. 

Tags