Maduro: Venezuela ina Rais mmoja tu
(last modified Mon, 04 Feb 2019 07:49:51 GMT )
Feb 04, 2019 07:49 UTC
  • Maduro: Venezuela ina Rais mmoja tu

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa, nchi hiyo ina Rais mmoja tu na kwamba kitendo cha kiongozi wa kambi ya upinzani cha kujitangazia urais nchini humo, ni kinyume kabisa cha katiba.

Rais Maduro amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya LaSexta na kumtaka kiongozi wa upinzani, Juan Guaidó aache chokochoko na kuitumbukiza nchi hiyo katika fujo na vurugu kwa tamaa ya kusaidiwa na madola ya Magharibi.

Vile vile amesema, yuko tayari kufanya mazungumzo na wapinzani na kuwataka wazingatie vizuri wanayoyafanya na wasichukue hatua ambazo zitailetea matatizo Venezuela.

Juan Guaidó, kibaraka wa madola ya Magharibi nchini Venezuela

 

Aidha Rais Maduro amepinga muda uliowekwa na baadhi ya nchi za Ulaya wa kuitishwa uchaguzi mwingine nchini humo. Baadhi ya nchi za Ulaya zimetishia kumtambua Juan Guaidó kuwa rais wa Venezuela kama hakutafanyika uchaguzi mwingine wa rais, suala ambalo linahesabiwa kuwa ni uingiliaji wa wazi na wa moja kwa moja wa masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Katika hatua inayokinzana na sheria zote za kimataifa na inayoonesha misimamo ya kindumilakuwili ya nchi za Maghari, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinamuunga mkono moja kwa moja Juan Guaidó aliyejitangazia urais wa Venezuela, kinyume kabisa na katiba ya nchi hiyo.

Serikali ya Rais Nicolas Maduro imechaguliwa kidemokrasia nchini Venezuela, hata hivyo kutokana na misimamo yake ya kutokubali kuburuzwa na madola ya Magharibi, nchi hizo za kibeberu zikiongozwa na Marekani zinachukua hatua mbalimbali zinazokanyaga sheria za kimataifa, ili kuitumbukiza kwenye matatizo nchi hiyo.

Tags