Mgawanyiko katika Umoja wa Ulaya kuhusu kadhia ya Venezuela
(last modified Tue, 05 Feb 2019 06:47:39 GMT )
Feb 05, 2019 06:47 UTC
  • Mgawanyiko katika Umoja wa Ulaya kuhusu kadhia ya Venezuela

Kufuatia kushadidi mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela, Umoja wa Ulaya umekuwa ukifuata sera za Marekani za kumpinga Rais Nicholas Maduro wa nchi hiyo na kumuunga mkono kiongozi wa upinzani.

Juan Guaido, aliyeondolewa kama Spika wa Kongresi ya Kitaifa ya Venezuela, mnamo Januari 23 alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela na baada ya hapo alikula kiapo kinyume cha sheria. Hatua hayo hiyo ya ukiukaji sheria iliungwa mkono na Marekani na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya.

Hivi sasa kumeibuka mgawanyiko katika umoja huo kuhusu namna ya kukabiliana na mgogoro wa Venezuela. Hii ni baada ya Italia kuzuia taarifa rasmi ya Umoja wa Ulaya ya kumtambua kinara wa upinzani, Guaido, kuwa 'rais' wa Venezuela.

Katika kikao kisicho rasmi cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kilichofanyika hivi karibuni huko Bucharest nchini Romania, Italia ilitumia kura yake ya turufu kupinga tangazo la Umoja wa Ulaya kumtambua Juan Guaido kama rais wa Venezuela. Hadi sasa Italia haijatangaza rasmi kuwa ilipinga taarifa hiyo lakini kabla ya kikao hicho naibu waziri wa mambo ya nje wa Italia alikuwa ametangaza bayana kuwa nchi yake haitamtambua Guaido kama rais wa Venezuela.

Hivi karibuni Umoja wa Ulaya ulikuwa umeitaka Venezuela iandae upya uchaguzi wa rais. Ufaransa na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya siku ya Jumamosi zilimuonya Maduro kuwa  kama hangeitisha uchaguzi wa Mapema kufikia Jumapili iliyopita, basi zingemtambua rasmi Juan Guaido kuwa rais wa Venezuela.

Rais Maduro wa Venezuela

Maduro alitupilia mbali agizo hilo la Umoja wa Ulaya na kusema Venezuela iko tayari kukabiliana na hujuma yoyote ile ya kigeni. "Kuhusu mashinikizo ya Ulaya ya kufanyika uchaguzi , Maduro amesema: "Ni kwa nini Umoja wa Ulaya unataka uchaguzi ufanyike tena? Ni kwa sababu muitifaki wao wa mrengo wa kulia hakushinda."

Uingereza, Uhispania, Ufaransa na Sweden, katika hatua ya uingiliaji kati masuala ya nchi nyingine, zimemtambua Guaido kuwa "rais wa muda wa Venezuela".

Hatua hii imepingwa vikali na Russia. Siku ya Jumatatu, Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, ilitangaza kuwa, mgogoro wa Venezuela unaweza kutatuliwa tu na watu wa nchi hiyo. Aidha Kremlin imekosoa  hatua ya nchi za Ulaya ya kuingilia mambo ya ndani ya Venezuela. "Kwa mujibu wa Dmitry Peskov, Msemaji wa Kremlin: "Jitihada za kupatia uhalali hatua za kunyakua madaraka Venezuela ni uingiliaji wa wazi na wa moja kwa moja wa masuala ya ndani ya nchi nyingine."

Hatua ya Umoja wa Ulaya ya kushirikiana na Marekani katika kuishinikiza serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela na rais halali wa nchi hiyo, Nicholas Maduro, ni jambo linalokumbusha namna baadhi ya nchi za Ulaya zilivyoshirikiana na Marekani katika mgogoro wa Syria.

Ikumbukwe kuwa tokea mwaka 2011 wakati mgogoro wa Syria ulipoanza, Ufaransa na Uingereza zilijiunga na njama za Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kujaribu kuiangusha serikali halali ya Syria inayoongozwa na Bashar al Assad. Nchi hizo hata ziliiunda makundi ya kigaidi ili kuiangusha serikali ya Syria lakini hatimaye zilishindwa.

Juan Guaido kinara wa upinzani Venezuela anayepata himaya ya baadhi ya madola ya Magharibi

Hali sawa na hiyo hivi sasa inajirudia nchini Venezeula ambapo nchi za Ulaya zinaipuuza serikali halali na rais aliyechaguliwa na wananchi na kumtambua kinara wa upizani, Guaido, kama rais wa Venezuela.

Hatua hii si tu kuwa ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya Venezeula, bali ni kinyume cha irada ya wananchi wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Hivi sasa nchi za Magharibi, yaani Marekani na Umoja wa Ulaya, zinatumia mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na hata zinalenga kutumia nguvu za kijeshi ili kumfanya Guaido awe rais wa Venezeula. Katika hali kama hiyo, hatua ya Italia kutumia kura yake ya turufu kuzuia Umoja wa Ulaya kumtambua kinara huyo wa upinzani wa Venezuela kama rais ni jambo ambalo limeibua nyufa na mgawanyiko mkubwa katika umoja huo.

Tags