Kushadidi makabiliano ya kisiasa nchini Venezuela
(last modified Wed, 13 Feb 2019 02:29:47 GMT )
Feb 13, 2019 02:29 UTC
  • Kushadidi makabiliano ya kisiasa nchini Venezuela

Matukio ya kisiasa nchini Venezuela yamefikia katika hatua nyeti kiasi kwamba, Rais Nicolas Maduro ametoa amri ya kufanyika manuva makubwa ya kijeshi ambayo ni ya kihistoria katika nchi hiyo.

Katika upande mwingine, Marekani na washirika wake wangali wanazungumzia kile wanachokitaja kuwa chaguo la kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na Rais Maduro pamoja na serikali yake ya mrengo wa kushoto.

Katika fremu hiyo, kutumwa misaada eti ya kibinadamu ya Washington umekuwa ulingo mkuubwa wa mzozo na makabiliano ya kisiasa baina ya kiongozi wa upinzani Juan Guaido na Rais Nicolas Maduro. Katika siku za hivi karibuni, suala la kutumwa misaada eti ya kibinadamu ya Marekani na hatua ya serikali ya Maduro ya kuzuia kuingia nchini humo misaada hiyo, limegeuzwa na kutumiwa na Juan Guaido na madola ya Magharibi kama wenzo wa kupiga ngoma ya vita dhidi ya Venezuela.

Maandamano ya kumuunga mkono Rais Nicolas Maduro

Kwa mtazamo wa Juan Guaido kiongozi wa upinzani nchini Venezuela ambaye alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo ni kuwa, misaada eti ya kibinadamu ya Marekani inaweza kwa kiwango kikubwa kulipatia ufumbuzi tatizo la uhaba wa dawa na chakula nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, mgogoro wa sasa wa kiuchumi wa Venezuela ni matokeo ya siasa za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya Venezuela na vikwazo vya Washington dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Ni kwa muda sasa ambapo Marekani imezidisha vikwazo vyake dhidi ya Venezuela na vikwazo hivyo vimeifanya nchi hiyo ikabiliwe na matatizo makubwa ya kiuchumi. Kwa mujibu wa ripoti ya chuo kimoja cha masuala ya kiistratejia na kijiopolitiki cha Amerika ya Latini ni kuwa, mbinyo wa kifedha ambao Marekani iliiwekea Venezuela baina ya mwaka 2013 hadi 2017, umesababisha hasara ya kati ya dola bilioni 260 hadi 350 kwa uchumi wa nchi hiyo. Kadhalika mbinyo huo umekifanya kiwango cha uzalishaji ghafi ndani ya Venezuela kupungua kwa baina ya asilimia 1.01 na 1.06. Kwa maneno mengine ni kuwa, vikwazo na mibinyo wa Marekani katika kipindi cha kati ya mwaka 2013 na 2017 ulisababisha hasara ya karibu dola 14,000 kwa kila mwanaume, mwanamke na mtoto wa Venezuela.

Rais Nicolas Maduro

Bi Delcy Rodriguez, Makamu wa Rais wa Venezuela ameiambia televisheni ya Russia Today kwamba: Uamuzi wa Washington wa kutuma eti misaada ya kibinadamu nchini Venezuela ni wa ria na wa kinafiki, kwa sababu vikwazo vya kiuchumi vya Marekani ndivyo vilivyoitumbukiza Venezuela katika mazingira haya mabaya ya kiuchumi. Misaada hiyo ya kibinadamu ni urongo mkubwa. Kile ambacho Venezuela inakihitajia filihali ni mazungumzo ya kitaifa baina ya serikali na wapinzani, kitu ambacho Marekani inakizuia.

Hivi sasa Marekani ikimuunga mkono Juan Guaido na ikitekeleza ombi lake, imetuma kifurushi cha misaada ya dawa na chakula. Hata hivyo, serikali ya Venezuela imekataa kuruhusu misaada hiyo kuingizwa nchini humo. Jeshi la Venezuela likitekeleza amri ya Rais Maduro limejikita katika mpaka wa nchi hiyo na Colombia ili lizuie kuingia nchini humo vifurushi hivyo vinavyotiliwa shaka. Wananchi wa Venezuela nao wamekusanyika katika maeneo hayo ya mpakani na kupiga nara dhidi ya siasa za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Kwa mtazamo wa Rais Maduro na serikali yake ni kuwa, kutumwa vifurushi vya misaada kama hiyo ni maonyesho na mchezo wa kuigiza ambao lengo lake ni kuandaa mazingira ya kutumwa wanajeshi nchini humo na kuanzisha vita.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani wa Venezuela aliyejitangazia Urais

Akizungumza tarehe 10 ya mwezi huu wa Februari, Rais Nicolas Maduro aliwaambia waandishi wa habari kwamba, misaada eti ya kibinadamu ya Marekani kwa Venezuela ina "sumu" na akazuia kuingia misaada hiyo katika nchi yake. Maduro aliituhumu Marekani kwamba, inafanya njama za kutokomeza uhuru na mamlaka ya kitaifa ya Venezuela kwa kisingizio cha kutuma misaada ya kibinadamu na kusema kuwa: Misaada ya Marekani ni pazia la kufunika jinai za Washington.

Licha ya kuwa, juhudi za Juan Guaido kiongozi wa upinzani wa Venezuela anayepata uungaji mkono na himaya ya Marekani na waitifaki wake zingali zinaendelea, lakini inaonekana kuwa, Rais Maduro akiwa pamoja na wananchi na vilevile jeshi la nchi hiyo na akiwa ameshikamana na malengo matukufu ya chuki dhidi ya ukoloni na dhidi ya Marekani, ameendelea na vita vyake dhidi ya Washington na vibaraka wake ndani ya Venezuela.

Tags