Umoja wa Ulaya waitaka Pakistan ichukue hatua za kuwashughulikia magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51788-umoja_wa_ulaya_waitaka_pakistan_ichukue_hatua_za_kuwashughulikia_magaidi
Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Pakistan ichukue hatua za wazi na endelevu dhidi ya makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2019 12:08 UTC
  • Umoja wa Ulaya waitaka Pakistan ichukue hatua za kuwashughulikia magaidi

Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Pakistan ichukue hatua za wazi na endelevu dhidi ya makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya imeeleza kuwa, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa umoja huo amefanya mazungumzo na Khurshid Mahmud Kasuri, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan na kusisitiza juu ya udharura wa serikali ya Islamabad kuchukua hatua za kudumu na za wazi dhidi ya makundi ya kigaidi ambayo yamo katika orodha ya Umoja wa Mataifa.

Kufuatia shambulio ya kigaidi la hivi karibuni mashariki mwa Iran, serikali ya Tehran iliitaka serikali na jeshi la Pakistan ikabiliane kwa nguvu zake zote na harakati za makundi ya kigaidi ya nchi hiyo katika mpaka wake na Iran.

Mahala palipotokea shambulio la kigaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchistan tarehe 13 Februari

Itakumbukwa kuwa, Februari 13, basi lililokuwa limewabeba askari walinda mpaka wa Iran lilishambuliwa na magaidi lilipokuwa likipita katika barabara ya Khash-Zahedan katika mkoa wa Sistan na Baluchistan, kusini mashariki mwa Iran, ambapo askari 27 waliuawa shahidi na wengine 13 walijeruhiwa.

Kundi la kigaidi linalojiita "Jayshul Adl" lilidai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi. Kundi hilo lina mfungamano mkubwa na magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na kufadhiliwa na serikali ya Saudi Arabia.