Antonio Guterres: Haki za Binadamu ulimwenguni zimo katika hali ya kutoweka
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonyesha kuchukizwa na suala la kuongezeka chuki dhidi ya wahajiri, ubaguzi na kupungua kiwango cha watu kustahamiliana.
Antonio Guterres amesema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, zaidi ya waandishi habari na waharakati 1000 wa masuala ya haki za binadamu wameuawa.
Ameongeza kuwa, binafsi anaamini kuwa, hali ya haki za binadamu ulimwenguni imo katika mkondo wa kudhoofika.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, katika mwaka uliopita wa 2018 kwa wastani kila wiki wanaharakati wanne wa masuala ya mazingira waliuawa.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo, Antonio Guterres amesema kuwa, kuna ulazima wa kufanyika juhudi zaidi kuwatetea watu wanaofanya kazi katika uga wa masuala ya haki za binadamu.
Aidha Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu ongezeko la umasikini ulimwenguni.
Guterres amesema, umasikini ni moja ya masuala hatari mno ambayo yanahatarisha suala la haki za binadamu.
Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kwamba, dhulma, kukosekana ajira, ukosefu wa usawa na kuzidi kuwa mbaya hali ya maisha ni mambo ambayo yamechangia kuibuka machafuko na mapigano katika maeneo mbalimbali.