Rais Maduro: Marekani sasa inafanya njama za kuanzisha vita Venezuela
(last modified Wed, 27 Feb 2019 04:45:48 GMT )
Feb 27, 2019 04:45 UTC
  • Rais Maduro: Marekani sasa inafanya njama za kuanzisha vita Venezuela

Rais Nicolás Maduro wa Venezuela amesema kuwa hivi sasa serikali ya Marekani inafanya njama za kuwasha moto wa vita katika eneo la Amerika ya Latini hususan nchini Venezuela.

Maduro ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya ABC News na kusisitiza kwamba pamoja na najama hizo, hatua zote za Marekani zitaishia kufeli. Katika mahojiano hayo ya kwanza ya Rais Nicolás Maduro na televisheni ya Kimarekani baada ya miaka kadhaa, ameongeza kuwa, Washington inakusudia kuibua mgogoro mkubwa wenye lengo la kuhalalisha kuingilia kijeshi nchini Venezuela na kuwasha moto wa vita ndani ya eneo la Amerika Kusini.

Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani Venezuela aliyejitangaza kuwa rais

Venezuela ilitumbukia katika mzozo wa kisiasa mwishoni mwa mwezi jana baada ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi  hiyo. Hatua hiyo iliyotekelezwa tarehe 23 Januari 2019, iliungwa mkono na Marekani na nchi za Ulaya, huku serikali ya Caracas ikiitaja kuwa ni sawa na tangazo la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Nicolás Maduro. Licha ya uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani na kambi ya Magharibi kwa Juan Guaidó, lakini raia na jeshi la Venezuela pamoja na mataifa kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Mexico, Uturuki, Afrika Kusini na Italia yameendelea kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro anayetambulika kisheria.

Tags