Kiongozi wa upinzani Venezuela anakabiliwa na kifungo cha miaka 30 jela
(last modified Wed, 27 Feb 2019 08:04:11 GMT )
Feb 27, 2019 08:04 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Venezuela anakabiliwa na kifungo cha miaka 30 jela

Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani aliyejitangaza kuwa rais wa mpito wa Venezuela anaandamwa na kifungo cha miaka 30 jela.

Hayo yamesemwa na Juan Carlos Valdez, Naibu Jaji wa Jopo la Haki la Mahakama ya Juu nchini humo katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik la Russia na kuongeza kuwa, hatua ya Guaido ya kwenda Colombia mnamo Februari 22 ilikiuka agizo la kumtaka asitoke nje ya nchi, lililotolewa na Mahakama ya Juu nchini humo, na hivyo amejiweka katika hatari ya kufungwa miaka 30 jela.

Amefafanua kuwa, "Guiado ni mtu anayekwepa sheria. Kitendo cha kutoroka nchini kinyume cha sheria na kisha kurejea hukumu yake ni kifungo cha hadi miaka 30 jela."

Venezuela ilitumbukia katika mzozo wa kisiasa mwishoni mwa mwezi jana baada ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi  hiyo.

Rais Nicolás Maduro wa Venezuela

Hatua hiyo iliyotekelezwa tarehe 23 Januari 2019, iliungwa mkono na Marekani na nchi za Ulaya, huku serikali ya Caracas ikiitaja kuwa ni sawa na tangazo la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Nicolás Maduro.

Licha ya uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani na kambi ya Magharibi kwa Juan Guaidó, lakini raia na jeshi la Venezuela pamoja na mataifa kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Mexico, Uturuki, Afrika Kusini na Italia wameendelea kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro anayetambulika kisheria.

Tags