Theresa May: Huenda hatutaondoka Umoja wa Ulaya
Waziri Mkuu wa Uingereza amedhihirisha msimamo mpya ambapo amesema kuwa kuna uwezekano nchi hiyo isijitoe katika Umoja wa Ulaya.
Theresa May jana alisema hivi na hapa ninamnukuu" kuna uwezekano tusiondoke kwa miezi kadhaa katika Umoja wa Ulaya. Hatuwezi kutoka katika Umoja wa Ulaya bila ya dhamana ambazo zimeonekana katika rasimu ya makubaliano ya Brexit na au kabisa tusitoke ndani ya Umoja wa Ulaya".
Theresa May aliongeza kuwa wiki ijayo wabunge wa bunge la Uingereza watakuwa na uchaguzi muhimu ambapo watapaswa kuunga mkono mapatano ya Brexit au kuyapinga. Waziri Mkuu wa Uingereza alisema kuwa iwapo wabunge hao wataunga mkono mapatano hayo basi Uingereza itajiondoa ndani ya Umoja wa Ulaya kama ilivyopangwa, lakini iwapo wabunge watapinga muafaka huo hakuna ajuaye kitakachojiri.
Waziri Mkuu wa Uingereza tarehe 12 mwezi huu anatazamiwa kuwasilisha bungeni kwa mara ya pili rasimu ya mapatano ya Brexit ili kupigiwa kura.