Mar 17, 2019 04:26 UTC
  • Maandamano makubwa yafanyika London kupinga ubaguzi

Makumi ya maelfu ya watu walikusanyika kati kati ya mji mkuu wa Uingereza, London jana Jumamosi kulaani na kupinga chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na ubaguzi wa rangi.

Maandamano  hayo yaliandaliwa na jumuiya ya kupinga ubaguzi inayojulikana kama Stand Up to Racisim na yalihudhuriwa na mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali, NGO, ya Waislamu pamoja na makundi mengine ya kupinga ubaguzi. Washiriki wamelaani vikali hujuma za kigaidi dhidi ya misikiti miwili nchini New Zealand zilizopelekea Waislamu wasiopingua 49 kuuawa.

Maandamano hayo ambayo awali yalikuwa yamepangwa kufanyika Machi 21 kwa munasaba Siku ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi Duniani yameitishwa kufuatia hujuma za kigaidi dhidi ya misikiti Ijumaa mjini Christchurch, New Zealand.

Maelfu ya washiriki waliandamana kutoka Bustani ya Hyde hadi katika Ofisi ya Waziri Mkuu katika Barabara ya Downing na pia walifika mbele ya ubalozi wa New Zealand mjini London kutoa heshima zao kwa waliouawa.  Waandamanaji wametuma ujumbe wa kufungamana na Waislamu kufuatia mauaji ya kinyama mjini Christchurch na kusema hujuma hiyo imeishtua dunia na ni kengele ya hatari kutokana na kuongezeka ugaidi wa wazungu wabaguzi wa rangi wenye misimamo ya kufurutu ada wa mrengo wa kulia.

Hali baada ya mauaji msikitini nchini New Zealand

Siku ya Ijumaa kulitokea shambulio la kutisha la kigaidi dhidi misikiti miwili ya Linwood na Al-Noor katika mji wa Christchurch nchini New Zealand dhidi ya Waislamu waliokuwa wanasali Sala ya Ijumaa. Katika hujuma hiyo ya kinyama Waislamu 49 waliuawa na wengine 50 walijeruhiwa vibaya, baadhi wakiwa mahututi. Nchi nyingi duniani na asasi za kimataifa hadi sasa zinaendelea kulaani shambulizi hilo.

Mtekelezaji mkuu wa ukatili huo ametambuliwa kuwa gaidi raia wa Australia mwenye misimamo mikali ya ubaguzi, Brenton Tarrant, ambaye ni mfuasi sugu wa Rais Donald Trump wa Marekani aliye maarufu kwa misimamo yake dhidi ya Uislamu.

Tags