Mamia ya Wamarekani waandamana mbele ya White House kumtetea Maduro
(last modified Sun, 17 Mar 2019 17:05:02 GMT )
Mar 17, 2019 17:05 UTC
  • Mamia ya Wamarekani waandamana mbele ya White House kumtetea Maduro

Mamia ya wananchi wa Marekani wamefanya maandamano mbele ya Ikulu ya Rais wa nchi hiyo, White House na kutangaza uungaji mkono wao kwa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro.

Ripoti zinasema mamia ya Wamarekani wamekusanyika katika Medani ya Lafayette karibu na Ikulu ya White House mjini Washington ambapo pamoja na kutangaza uungaji mkono wao kwa Rais Maduro wa Venezuela, wamewataka viongozi wa Marekani wakome kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Waandamanaji hao pia wametaka kufutwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela na kutupilia mbali kabisa uamuzi wa aina yoyote wa kutuma majeshi ya Marekani huko Venezuela.

Maandamano hayo pia yamelaani njama zinazofanywa na Marekani za kutaka kumsimika madarakani Juan Guaido badala ya Rais wa sasa wa Venezuela, Nicolas Maduro. 

Maandamano kama hayo ya kumuunga mkono Maduro yamefanyika pia katika miji mingine kadhaa ya Marekani kama New York na Los Angeles.

Itakumbukwa kuwa, Rais Nicolas Maduro alishinda uchaguzi wa rais uliofanyika kidemokrasia mwezi Mei mwaka jana nchini Venezuela na kuidhinishwa kutawala nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka 6.  

Venezuela ilitumbukia katika mzozo wa kisiasa mwishoni mwa mwezi Januari baada ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi  hiyo. Hatua hiyo iliungwa mkono na Marekani na nchi za Ulaya, huku serikali ya Caracas ikiitaja kuwa ni sawa na tangazo la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Nicolás Maduro. 

Tags