Marekani: Saudia inaongoza kwa kukiuka uhuru wa kuabudu
(last modified Tue, 30 Apr 2019 12:22:49 GMT )
Apr 30, 2019 12:22 UTC
  • Marekani: Saudia inaongoza kwa kukiuka uhuru wa kuabudu

Kamisheni ya Kimataifa ya Kutathmini Uhuru wa Kuabudu ya Marekani (USCIRF) imeitaja Saudi Arabia kama moja ya nchi zinazoongoza duniani kwa kukiuka uhuru wa kuabudu.

Katika ripoti yake ya mwaka huu 2019 iliyotolewa jana Jumatatu, kamisheni hiyo ya serikali ya Marekani imesema Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaendelea kuandamwa na ubaguzi katika sekta za elimu, ajira, Idara ya Mahakama, na kunyimwa nafasi za juu serikalini au katika jeshi.

Kamisheni hiyo imesema ilitembelea mkoa wa mashariki mwa nchi ambao aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia na kuwahoji, ambapo walisema kuwa wanadhalilishwa na kukandamizwa na maafisa usalama.

Ripoti ya Kamisheni ya Kimataifa ya Kutathmini Uhuru wa Kuabudu ya Marekani kadhalika imekosoa kitendo cha utawala wa Aal-Saud cha kukiuka uhuru wa kuabudu wa watu wa dini nyinginezo, sambamba na kuwafanyia ubaguzi wanawake na kuwakandamizi wafungwa wa itikadi. 

Waislamu wakiandamana kulaani mauaji ya Sheikh Nimri Baqir an-Nimr, mwanazuoni mkubwa wa Waislamu wa Shia aliyeuawa kwa kukatwa kichwa na Aal-Saud mashariki mwa Saudia

Ripoti hiyo ya USCIRF imetolewa siku chache baada ya watawala wa Aal-Saud kuwanyonga kwa kuwakata vichwa watu 37, aghalabu yao wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na kisha kuanika mwili wa mmoja wa Waislamu hao waliowafanyia ukatili huo hadharani kwa ajili ya kutazamwa na umati.

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa taasisi za kimataifa zilizitoa taarifa za kulaani ukatili huo.