Russia yalaani uingiliaji haribifu wa Marekani nchini Venezuela
(last modified Thu, 02 May 2019 06:34:56 GMT )
May 02, 2019 06:34 UTC
  • Russia yalaani uingiliaji haribifu wa Marekani nchini Venezuela

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amelaani vikali uungaji mkono haribifu wa Marekani kwa kinara wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido ambaye alikuwa amedai amepata uungaji mkono wa jeshi katika jaribio lililofeli la kumpindua Rais Nicolas Maduro.

Lavrov aliyasema hayo Jumatano wakati akizungumza kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ambapo amemfahamisha bayana kuwa, uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezeula ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Lavrov aidha amekosoa vitisho vya wakuu wa Marekani hasa Rais Donald Trump kuhusu kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Rais Maduro na kusema, utekelezwaji wa hatua kama hizo utakuwa na matokeo mabaya.

Mapema Jumanne Caracas, mji mkuu wa Venezuela ulishuhudia vurugu baada ya kundi dogo la wanajeshi kujiunga na Juan Guaido katika jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya mrengo wa kushoto inayoongozwa na Nicolas Maduro. Baada ya masaa machache Rais Maduro alihutubia taifa kwa njia ya televisheni na kutangaza kuwa jaribio hilo la mapinduzi limesabaratishwa.

Sergei Lavrov (kushoto) na Mike Pompeo

 

Ikumbukwe kuwa, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais, Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela hapo tarehe 23 Januari mwaka huu kupitia uungaji mkono kamili wa Marekani na washirika wa Washington. Hata hivyo licha ya njama hizo za kutaka kumuondoa madarakani Rais Maduro, jeshi na wananchi pamoja na nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Afrika Kusini na mataifa mengi ya dunia yameendelea kusisitizia ulazima wa kuheshimiwa haki ya kujitawala nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

 

Tags