Udharura wa ulimwengu uliostaarabika kusimama mbele ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53550-udharura_wa_ulimwengu_uliostaarabika_kusimama_mbele_ya_marekani
Akiwa katika safari ya kuitembelea Japan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza na viongozi wa nchi hiyo kuhusu mapatano ya nyuklia mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, na vile vile siasa haribifu za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
May 18, 2019 03:21 UTC
  • Udharura wa ulimwengu uliostaarabika kusimama mbele ya Marekani

Akiwa katika safari ya kuitembelea Japan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza na viongozi wa nchi hiyo kuhusu mapatano ya nyuklia mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, na vile vile siasa haribifu za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Akizungumza na waandishi habari siku ya Alkhamisi mara tu baada ya mazungumzo hayo mjini Tokyo, Muhammad Jawad Zarif alisema: Ulimwengu uliostaarabika unapasa kusimama imara mbele ya ubabe wa utawala wa Marekani ambao unawapinga watu wanaoheshimu sheria na kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Huku akisema kuwa harakati haribifu za Marekani zimeongezeka maradufu baada ya kutimia mwaka mmoja wa kujiondoa nchi hiyo katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA, Waziri Zarif amesema kwamba ameanzisha juhudi kubwa za kufanya mazungumzo na nchi muhimu za dunia kwa lengo la kuzuia kuongezeka mivutano iliyopo. Hata hivyo amesema kwamba suala hilo halina maana ya Jamhuri ya Kiislamu kufumbia macho haki na maslahi yake ya kitaifa na kwamba licha ya kuipa kipaumbele nafasi ya udiplomasia lakini itaendelea kuyatetea maslahi yake hayo ya kitaifa kwa nguvu zake zote. Iran daima imekuwa ikipinga kuwepo mivutano katika eneo la kistratijia la Asia Magharibi na hatua zake mpya katika fremu ya JCPOA pamoja na safari ya Zarif katika nchi za Asia, ni alama na dalili tosha kwamba nchi hii ina nafasi chanya na inatekeleza vilivyo majukumu yake katika ngazi za kimataifa. Siasa za msingi za Iran katika upeo wa siasa za nje ni kufanya mazungumzo chanya ma kushirikiana na mataifa mengine kwa ajili ya kutatua matatizo muhimu na kuheshimiwa sheria za kimataifa na za Umoja wa Mataifa. Kujukumika Iran katika utekelezaji wa ahadi zake za mapatano ya JCPOA, katika kilele cha hatua haribifu za Marekani kuhusiana na mapatano hayo ya kimataifa, ni jambo linalothibitisha wazi uwajibikaji wa Iran katika ngazi za kimataifa.

Waziri Muhammad Jawad Zarif akiwasili mjini Tokyo kwa mazungumzp na viongozi wa Japan

Kuzidishwa mashinikizo dhidi ya taifa la Iran, mivutano zaidi katika eneo la Asia Magharibi na vitisho pamoja na kuadhibiwa na Marekani nchi zinazoshirikiana kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni baadhi ya dalili zinazoonyesha wazi ubeberu na ubabe wa nchi hiyo, ambao ni hatari kubwa kwa usalama na amani ya dunia. Baada ya Donald Trump kuingia madarakani nchini Marekani, sheria, mfumo wa utawala wa pande kadhaa na mapatano ya kimataifa yamekuwa yakikabiliwa na hatari kubwa, ambapo kuna uadharura wa jamii ya kimataifa kukabiliana vilivyo na tabia hizo za ubabe wa Marekani.

Siasa na mienendo ya chuki ya utawala wa Trump dhidi ya Iran ni ya kisiasa moja kwa moja na hatua ambazo umekuwa ukizitekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na baada ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA zinathibitisha wazi ukweli huo. Kuhusiana na hilo, Mkuu wa Kamati ya Habari, Masuala ya Kigeni na Majeshi ya Kongresi ya Marekani amemwandikia barua Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo akielezea mawasiwasi wake na vilevile kumtahadharisha dhidi ya kutumia vibaya na kisiasa habari za intelijensia kuhusu Iran. Sehemu ya barua hiyo inasema: Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani aghalabu hutumia kisiasa habari za intelijensia kuhusu Iran.

Wakati huo huo, Bernie Sanders na Chris Van Hollen, Maseneta wawili wa Marekani wamemwambia Trump kupitia ujumbe: Mwenendo wa serikali ya Marekani kuhusiana na Iran utakuwa na matokeo kinyume na inavyotarajiwa. Tim Kaine Seneta mwingine wa Marekani wa Chama cha Democrat anasema: 'Sisi tunaamini kwamba kuingia kwenye vita na Iran utakuwa ni upumbavu.'

Trump akiwa na timu yake ya vita na mivutano White House, Bolton (kushoto) na Mike Pompeo

Sauti hizi za wapinzani zinaonyesha kwamba ndani ya Marekani pia kuna watu wenye busara ambao wanakerwa na tabia na siasa haribifu za utawala wa Trump na timu yake ya vita. Harakati mpya za Marekani katika eneo la Asia Magharibi zinatokana na habari za intelijensia zilizojaa makosa, na kwa kauli ya vyombo vya habari vya Marekani, hatua za Iran katika eneo ni za kujilinda tu. Kuhusiana na suala hilo, gazeti la Wall Street Journal limewanukuu maafisa kadhaa wa serikali ya Trump na kuandika: Habari mpya za intelijensia kuhusu Iran zinaonyesha kwamba Wamarekani wamekosea katika kutafsiri harakati za Tehran, na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na kile kinachotajwa kuwa ni hatari kutoka Iran, ni za kujilinda tu.

Kupewa kipaumbele nafasi ya udiplomasia na sheria za kimataifa bila shaka kutaweka wazi harakati za kichochezi na za kupenda vita za watawala wa hivi sasa wa Marekani pamoja na waungaji mkono wao kadhaa katika eneo la Asia Magharibi. Bila shaka jambo hilo litazipelekea nchi nyingine huru za dunia kuchukua msimamo wa wazi dhidi ya tabia na mienendo haribifu ya Marekani katika ngazi za kimataifa. Ni wazi kuwa hilo ni moja ya malengo ya safari ya ya hivi sasa ya Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi kadhaa muhimu za Asia, zikiwemo Japan, India na China.