May 27, 2019 07:12 UTC
  • Wanajeshi wa Myanmar waliowaua Waislamu wa Rohingya waliachiwa kabla ya muda

Imebainika kuwa, wanajeshi wa Myanmar waliowaua Waislamu wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine mwaka 2017, waliachiwa huru kabla ya kukamilisha vifungo vyao.

Hayo yamefichuliwa na shirika la habari la Reuters, baada ya kufanya mahojiano maalumu na maafisa wawili wa gereza, wafungwa wawili wa zamani na mmoja wa wanajeshi hao walioachiwa huru.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Reuters, wanajeshi saba wa Myanmar ambao walikuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kwa kuwaua Waislamu kumi wa jamii ya Rohingya katika operesheni yao dhidi ya kijiji cha Inn Din mkoani Rakhine mwaka 2017, waliachiwa huru Novemba mwaka jana, kwa maana kwamba hata hawakumaliza mwaka mmoja kati ya miaka kumi ya vifungo vyao.

Habari zaidi zinasema kuwa, wanahabari wawili wa Reuters waliofichua mauaji hayo Wa Lone na Kyaw Soe Oo ambao waliachiwa huru Mei 6, walitumikia vifungo virefu gerezani kuliko wanajeshi hao makatili, kwani walifungwa zaidi ya miezi 16 gerezani.

Waislamu wa jamii ya Rohingya kabla ya kuuawa kikatili na wanajeshi wa Myanmar

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limekuwa likitoa ripoti mara kwa mara zinazosema kuwa jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka 2017. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya Warohingya milioni moja kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ikiwemo Bangladesh.

Tags