WHO: Matumizi ya tumbaku yanaua watu milioni 8 kila mwaka duniani
Shirika la Afya Duniani WHO limesema watu zaidi ya milioni nane wanafariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku kote duniani, kutoka milioni saba mwaka 2017.
Katika taarifa aliyotoa kwa mnasaba wa Siku ya Dunia Bila ya Tumbaku inayoadhimishwa leo Ijumaa, na ambayo huadhimishwa tarehe 31 Mei kila mwaka, Vinayak Prasad, Mkurugenzi wa Magonjwa Yasiyoambukiza wa WHO amesema kuwa, asilimia 40 ya waathiriwa wa tumbaku wanapoteza maisha kutokana na ugonjwa wa mapafu.
Amesema watu karibu milioni moja wanaaga dunia kila mwaka kutokana na athari ya moshi wa wavuta sigara, wakiwemo watoto zaidi ya 60,000.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, kuna wavutaji sigara bilioni 1.1 duniani kote.
Taarifa ya WHO imesema kuwa, matumizi ya tumbaku mbali na kusababisha maafa, yanaongeza viwango vya umasikini, kupunguza ukuaji wa uchumi, kuvunja nyumba, mbali na kuchafua mazingira.
WHO imetahadharisha kuwa, yumkini watu bilioni moja watakuwa wamepoteza maisha kutokana na matumizi hayo ya tumbaku kufikia mwishoni mwa karne hii.