Idara ya Intelijensia ya Russia: Hakuna ushahidi kuwa al-Baghdadi ameuawa
Idara ya intelijensia ya masuala ya kigeni ya Russia (SVR) imesema kuwa hakuna nyaraka thabiti zinazothibisha kwamba Abubakar al-Baghdadi, Kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ameuawa.
Sergey Naryshkin, Mkuu wa Idara ya Intelejensia ya Masuala ya Kigeni ya Russia aliyasema hayo jana Ijumaa na kuongeza kwamba, hakuna taarifa za vijinasaba ambayo inaweza kuifanya Moscow iamini kuwa al-Baghdadi ameuawa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Marekani nchini Syria. Kabla ya hapo pia Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza kwamba hadi sasa hakuna taarifa za kuaminika zinazothibitisha kifo cha kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS).
Tarehe 27 mwezi jana Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kwamba kinara huyo wa (ISIS) aliuawa katika operesheni maalumu iliyotekelezwa na askari wa nchi hiyo huko katika mkoa wa Idlib, nchini Syria. Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) miaka ya hivi karibuni lilivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Iraq na Syria likisaidiwa na Marekani, Saudi Arabia, utawala wa Kizayuni wa Israel na washirika wao na kufanya jinai za kutisha katika nchi hizo na kwingineko duniani.