Homa ya mapafu (pneumonia) inaua mtoto mmoja katika kila sekunde 39
Taasisi za afya duniani zimeripoti kuwa, homa ya mapafu (pneumonia) inaua mtoto mmoja katika kila sekunde 39, na kwamba ugonjwa huo uliua watoto laki nane mwaka jana pekee.
Hayo yameripotiwa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef), shirika la kimataifa la Save the Children na taasisi nyingine nne za afya duniani katika ripoti yao mpya iliyotolewa leo Jumanne chini ya kaulimbiu inayosema "Janga Lililosahaulika".
Seth Berkley, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la GAVI amesema ni jambo la kusikitisha namna homa ya mapafu inavyoua watoto kwa kiasi hicho cha kutisha katika hali ambayo ni ugonjwa unaoweza kutambuliwa haraka, unaozuilika kwa chanjo na hata kutibika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nusu ya vifo hivyo laki nane vya watoto kutokana na ugonjwa wa pneumonia viliripotiwa katika nchi za Nigeria, India, Pakistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ethiopia, na kwamba aghalabu ya vifo hivyo vikiwakumba watoto walio chini ya umri wa miaka miwili.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Save the Children, Kevin Watkins, ametaja vifo hivyo kama janga la kimataifa linalohitaji hatua za dharura za jamii ya kimataifa ili kunusuru maisha ya mamilioni ya watoto.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya taasisi za afya duniani, homa ya mapafu inasababisha asilimia 15 ya vifo vya watoto duniani, hususan walio chini ya umri wa miaka mitano.