WHO: Malaria ingali tishio, yaua mtoto mmoja katika kila dakika 2
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema ugonjwa wa malaria ungali tishio kubwa linalowaathiri mamilioni ya watu kila mwaka kote duniani hususan katika nchi za Afrika.
WHO imetadharisha katika ripoti yake ya leo Jumatano kuwa, kasi ya kupambana na ugonjwa huu imepungua kwa kiasi cha kutisha, licha ya maradhi hayo kuua watu zaidi ya laki nne kila mwaka duniani hususan barani Afrika.
Pedro Alonso, mtaalamu wa malaria wa WHO amesema, "Kuna haja kwa nchi wadhamini na serikali katika nchi zilizoathiriwa na malaria kuongeza kasi ya kukabiliana na ugonjwa huu, kwani unaua mtoto mmoja katika kila dakika mbili."
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, wanawake milioni 11 wajawazito katika nchi za chini ya jangwa la Sahara barani Afrika, walikumbwa na malaria mwaka jana, na kupelekea watoto laki tisa wazaliwe wakiwa na uzani wa chini kupita kiasi na hivyo kuweka maisha ya watoto hao hatarini.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, thuluthi moja ya watoto wadogo katika nchi za chini ya jangwa la Sahara barani Afrika hadi kufikia mwaka jana 2018, walikuwa hawalali chini ya neti au vyandarua vilivyotibiwa.
Hii ni katika hali ambayo, Septemba mwaka huu, wataalamu wa masuala ya afya walisema kuwa ugonjwa wa malaria unaweza kutokomezwa kabisa duniani hadi kufikia mwaka 2050, siku chache baada ya Shirika la Afya Duniani kuchapisha ripoti yake iliyosema kuwa, haiwezekani kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria hivi karibuni.