Venezuela yaishukuru Iran kwa kuifikishia mafuta na kuvunja vikwazo vya Marekani
(last modified Mon, 25 May 2020 03:58:14 GMT )
May 25, 2020 03:58 UTC
  • Venezuela yaishukuru Iran kwa kuifikishia mafuta na kuvunja vikwazo vya Marekani

Mwakilishi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya meli ya kwanza ya mafuta ya Iran kuingia katika maji ya nchi hiyo na kusema kuwa, hii ni hatua muhimu sana katika kupambana na ubeberu wa Marekani na kupigania haki ya kujitawala, uhuru na amani.

Samuel Moncada aliandika hayo jana Jumapili katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na huku akigusia kufika meli ya kwanza ya mafuta ya Iran katika maji ya Venezuela ameandika: rais wa Marekani, Donald Trump na vitimbakwiri vyake, wanatishia kushambulia meli za mafuta za Iran wakati huu ambapo dunia nzima inakabiliana na janga la corona, lakini wataalamu wa mambo wanasema kuwa, Trump anatafuta kitu kingine, si hicho.

Meli ya kwanza ya mafuta ya Iran inayojulikana kwa jina la Fortune imeingia kwenye maji ya Venezuela ikisindikizwa na jeshi la majini na la anga la nchi hiyo.

Samuel Moncada, Mwakilishi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa

 

Meli moja ya kivita ya Marekani inayojulikana kwa jina la "Adam Joseph" ilikuwa inaifuata nyuma nyuma meli hiyo ya mafuta ya Iran lakini ilipoingia kwenye eneo maalumu la kiuchumi la Venezuela iliacha kufanya hivyo.

Vyombo vya habari vinasema kuwa, ukitoa meli hiyo ya Fortune, kuna meli nyingine nne za mafuta za Iran ziko njiani kuelekea nchini Venezuela hivi sasa.

Tarehe 14 mwezi huu wa Mei, Marekani ilisema kuwa inachunguza kuchukua hatua zinazofaa kujibu hatua hiyo ya Iran ya kuipelekea mafuta Venezuela.

Hata hivyo viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameionya vikali Marekani isijaribu kuzifanyia usumbufu wowote meli zake hizo kwani Tehran haitosita hata kidogo kutoa majibu makali wakati wowote itakapochokozwa.

Tags