Marekani yaitaka tena Korea Kaskazini ifumbie macho silaha za nyuklia
(last modified Wed, 27 May 2020 05:07:54 GMT )
May 27, 2020 05:07 UTC
  • Marekani yaitaka tena Korea Kaskazini ifumbie macho silaha za nyuklia

Kwa mara nyingine Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani ameitaka Korea Kaskazini ifumbie macho silaha za nyuklia kwa kile alichokiita kuwa ni kupewa fursa za kiuchumi.

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani sambamba na kuutaja kuwa muhimu ushiriki wa Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini katika kikao cha kijeshi na sisitizo lake la kuimarishwa uwezo wa silaha za nyuklia wa serikali ya Pyongyang, amesema kuwa ni bora kwa nchi hiyo kuachana na miradi yake ya nyuklia. Kadhalika O'Brien amesema kuwa iwapo Korea Kaskazini inataka kujiunga na jamii ya kimataifa na kunufaika na uchumi mkubwa, ni lazima itokomeze silaha zake za nyuklia na kuachana kabisa na miradi yake ya nyuklia. Baada ya kusimama kwa miezi kadhaa, kwa mara nyingine viongozi wa Marekani wameanzisha tena madai yao kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Korea Kaskazini. Katika miezi kadhaa ya hivi karibuni hasa baada ya kuenea kwa virusi hatari vya Corona nchini Marekani na kuibuka changamoto kubwa zinazomkabili Rais Donald Trump wa nchi hiyo kutokana na kufeli kwake katika kukabiliana na virusi hivyo na sambamba na kuibuka kwa tetesi za kufariki dunia Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini, viongozi wa White House walikuwa wamesitisha matamshi yao kuhusiana na suala la nyuklia la nchi hiyo ya Asia.

Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani

Tangu Trump aingie madarakani nchini Marekani mwaka 2016 hadi leo, daima amekuwa akifuata siasa za aina tofauti katika kuamiliana na kadhia ya nyuklia ya Korea Kaskazini. Wakati fulani, serikali ya Marekani hususan katika duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Trump na Kim Jong-un hapo mwezi Juni 2018 nchini Singapore ilitoa ahadi kwamba iwapo serikali ya Korea Kaskazini ingesitisha miradi yake ya silaha za nyuklia na majiribio ya makombora ya silaha hizo, basi mkabala wake Washington nayo ingeifutia nchi hiyo vikwazo ilivyoiwekea. Hata hivyo katika kipindi cha kati ya duru ya kwanza na ya pili ya mazungumzo kati ya viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini mwezi Februari mwaka 2019 huko mjini Hanoi, Vietnam, si tu kwamba White House haikuifutia vikwazo serikali ya Pyongyang, bali ilishadidisha vikwazo hivyo sambamba na kutekeleza stratijia ya uhasama dhidi ya Korea Kaskazini. Katika hali ambayo tangu mwanzo wa mazungumzo ya pande mbili Marekani ilikuwa ikizungumzia suala la kutoa fursa kadhaa kuhusiana na faili la nyuklia la Korea Kaskazini, lakini miezi michache baadaye siasa za nchi hiyo zilibadilika na kuwa za ubabe na vitisho vya moja kwa moja dhidi ya nchi hiyo ya Asia, hali iliyodhihiri wazi baada ya kufeli duru ya pili ya mazungumzo ya viongozi wa nchi mbili.

Kim Jong-un na Trump, katika mazungumzo ambayo hayakuzaa matunda

Baada ya Marekani kutotekeleza ahadi zake kuhusu Korea Kaskazini sambamba na kufuata stratijia za uhasama dhidi ya nchi hiyo, viongozi wa Pyongyang walianzisha majaribio ya makombora, suala ambalo lililipelekea kukosolewa vikali siasa za Trump kuhusiana na mzozo wa Rasi ya Korea. Pamoja na kushadidi vitisho vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini hasa baada ya kuanza kwa majaribio ya makombora ya nchi hiyo, lakini viongozi wa Pyongyang wanaamini kwamba ukakamavu na kusimama imara mkabala wa kupenda makubwa na utumiaji mabavu wa Marekani ndio njia pekee ya kukabiliana na siasa mbovu za White House. Hata pendekezo jipya la mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani kwa Korea Kaskazini kuhusiana na kufumbia macho miradi yake ya nyuklia mkabala wa kupewa fursa za kiuchumi, linamaanisha kwamba Washington imefikia natija hii kwamba ni lazima ibadilishe mwenendo wake wa hapo kabla. Kuhusiana na suala hilo Richard Haass, Mkuu wa Baraza la Uhusiano wa Kigeni nchini Marekani anasema kuwa: "Iwapo Rais Donald Trump atafuatilia siasa zake za zamani za uhasama, basi ni lazima ajiandae kwa kupta jibu kali kutoka Korea Kaskazini." Inaonekana kwamba pendekezo la Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani kwa kiongozi wa Korea Kaskazini kwa ajili ya kupata fursa za kiuchumi mkabala wa kuachana na miradi ya nyuklia, ni siasa mpya za 'mlingano sawa wa fursa', hasa baada ya kufeli kwa siasa za ubabe za nchi hiyo ya Magharibi mbele ya Korea Kaskazini.

Tags