Marekani na mwendelezo wa vikwazo vya mafuta dhidi ya Venezuela
(last modified Thu, 04 Jun 2020 02:29:55 GMT )
Jun 04, 2020 02:29 UTC
  • Marekani na mwendelezo wa vikwazo vya mafuta dhidi ya Venezuela

Marekani imeapa kuzidisha vikwazo na kuishinikiza zaidi serikali ya Venezuela licha ya kufeli siasa zake za vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Katika uwanja huu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema Washington imeyawekea vikwazo makampuni mengine manne ya mafuta ya Venezuela na ameitaka jamii ya kimataifa izidishe mashinikizo dhidi ya serikali ya Caracas hadi itakapoondolewa madarakani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amedai kuwa, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ndiye sababu ya mgogoro wa kibinadamu, kiuchumi na kisiasa wa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2019 Marekani ilianza kutekeleza vikwazo vya aina mbalimbali dhidi ya serikali ya Caracas ikiwemo vikwazo vya sekta ya nishati na mafuta kwa shabaha eti ya kuishinikiza serikali ya Venezuela na kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro anayepinga mfumo wa kibepari wa nchi za Magharibi. Katika mkondo huo Marekani ilipiga marufuku ununuzi wa mafuta ya Shirika la Mafuta la Taifa la Venezuela na ikatangaza kuwa, nchi au kampuni yoyote ya kigeni itakayonunua mafuta ya Venezuela itawekewa vikwazo na kuadhibiwa. Maafisa wa serikali ya Washington pia wamezidisha mashinikizo ya aina mbalimbali kwa sekta ya uchumi hususan biashara na mfumo wa benki wa Venezuela katika zoezi la kuzidisha matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo na kuwafagilia njia wapinzani wa Rais Nicolas Maduro.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, serikali ya Marekani inafanya jitihada za kusimika serikali tegemezi na kibaraka itakayolinda na kudhamini maslahi ya Washington katika mowajapo ya nchi muhimu zaidi za America ya Latini na hivyo kuzidisha satua na ushawishi wake katika eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela Jorge Arreaza anasema: Lengo na kuendelezwa mzingiro wa Washington dhidi ya nchi za America ya Latini na caribbean ni kuhodhi maliasili za eneo hilo na kuzisimika madarakani serikali zitakazolinda na kudhamini maslahi ya Marekani. Kwa msingi huo nchi za eneo hili daima zimekuwa zikilengwa kwa majaribio ya mapinduzi, uchochezi wa machafuko na ghasia, ugaidi, vita na mzingio wa kiuchumi, kibiashara na kifedha.

Licha ya mashinikizo hayo ya Marekani lakini Venezuela imefanikiwa kushinda vikwazo na vizingiti vya Marekani kutokana na siasa za Nicolas Maduro na msaada wa wananchi, jeshi na vilevile ushirikiano na nchi kama Iran, Russia na China. Suala hilo limezidisha hasira ya viongozi wa Marekani. Kuhusiana na suala hilo mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Bolton amekiri kuwa, Iran na China zinashirikiana na Venezuela kwa ajili ya kuifedhehesha Marekani. Hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutuma meli tano kubwa za mafuta huko Venezuela licha ya vitisho vilivyokuwa vimetolewa na Marekani imezidisha mara dufu hasira za viongozi wa serikali ya Washington. Kwa maneno mengine inatupasa kusema kuwa, kufika kwa meli hizo tano zinazobeba mafuta huko Venezuela ni tukio muhimu sana katika uwanja wa kuvunja siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu za Marekani dhidi ya nchi za Iran na Venezuela.   

Mwakilishi wa kudumu wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa Samuel Moncada amesema kuwa: "Kuwasili mafuta ya petroli ya Iran kwa wananchi wa Venezuela ni tukio muhimu sana katika njia ya mapambano ya kuwa huru, kujitawala na kuwa na amani. Donald Trump na vikaragosi wake wanafikiria kushambulia meli hizo za mafuta katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona.”

Kudhamini mafuta ya petroli ya Venezuela katika kipindi hiki cha kilele cha mashinikizo ya Marekani ni kielelezo cha kufeli siasa za Washington za kutaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Sasa viongozi wa Washington wanazungumzia suala la kuiwekea vikwazo vipya vya mafuta serikali ya Caracas. Inaonekana kuwa, lengo la hatua hii ni kutaka kuficha kipigo na kushindwa kwa siasa za vikwazo za Washington na baadaye kutimiza malengo yake ya kishetani na kibeberu, jambo ambalo pia litashindwa na kugonga mwamba.   

Tags