UN: Watoto bado wanatumiwa vitani duniani na haki zao zinakiukwa
Umoja wa Mataifa umesema janga la wavulana na wasicha kutumiwa na kufanyiwa ukatili kwenye mizozo ya silaha limeendelea kwa mwaka mzima wa 2019.
Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya 2019 kwenye Baraza la Usalama kuhusu Watoto na mizozo ya silaha , mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya watoto kwenye mizozo ya silaha Virginia Gamba amesema Umoja wa Mataifa umethibitisha na kuorodhesha zaidi ya vitendo 25,000 vya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto katika ripoti hiyo.”
Ameongeza kuwa kwa ujumla idadi ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto bado iko juu kama ilivyokuwa mwaka 2018 ambayo ni sawa na aina 70 za ukiukwaji kwa siku.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Katibu Mkuu maeneo yanayotia wasiwasi mkubwa ni Pamoja na Yemen, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, utawala wa Israel, Palestina na Syria.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umeliondoa jina la Saudi Arabia na washirika wake katika orodha ya makundi yanayokanyaga na kuvunja haki za watoto. Umoja wa Mataifa umetangaza habari hiyo sambamba na mashambulizi makali ya Saudi Arabia na washirika wake katika mkoa wa Saada huko kaskazini mwa Yemen ambayo yameua raia 12 wakiwemo wanawake na watoto wadogo kadhaa.
Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama vile Human Rights Watch na Save the Children yamemjia juu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kukosoa vikali uamuzi huo.