COP28: "Mustakabali wa watoto uko hatarini"
Watoto kutoka nchi za Kiafrika na Amerika Kusini jana Jumatano walizungumza katika mkutano wa kilele wa hali ya hewa, COP28 unaofanyika huko Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, wakitahadharisha kuhusu mustakbali wa watoto kote duniani.
Watoto hao wameonya kuwa mustakabali wao uko hatarini na kuwataka viongozi kuchukua hatua haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
"Mustakabali wa watoto uko hatarini," amesema Revan Ahmed mwenye umri wa miaka 13 kutoka Libya. "Tupo hapa kutetea mustakabali wetu kwa sababu mabadiliko ya tabianchi hayasababishwi na sisi, yamesababishwa na vizazi vilivyopita, lakini tunalipa gharama na tunaendelea kulipa. Hivyo ni haki yetu kutetea mustakabali wetu na kutaka kukomeshwa hali mabadiliko ya tabianchi.”
Akitoa mfano wa athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, Revan Ahmed ameashiria mafuriko yaliyoharibu mji wa Derna nchini Libya mapema mwaka huu na kuua zaidi ya watu 11,000.
Wakati huo huo, Lova Renee mtoto mwenye umri wa miaka 13 anasema nchi yake Madagascar imeathiriwa vibaya na mabadiliko ya hali ya hewa na kwamba watoto wameathirika pakubwa.
"Nchini Madagascar, tuna ukame na watoto wengi hawana maji, hawana chakula, wanaishia kufa, na hawana matumaini," Renee alisema.
Watoto hao wamezungumza katika halfa ya mkutano huo, wakati wawawilishi wa nchi mbalimbali wakijiandaa kwa wiki ya mwisho ya mazungumzo ambayo wanamazingira wanatumai yatapelekea kufikiwa makubaliano ya kukomesha matumizi ya fueli ya visukuku.
Katika wiki ya kwanza ya mkutano huo, kumepatikana baadhi ya mafanikio, hasa kuundwa mfuko wa "hasara na uharibifu" ili kufidia nchi zilizokumbwa na majanga ya hali ya hewa.