Apr 09, 2024 11:12 UTC
  • Utafiti wafichua: Wanawake Kenya wanageuzwa tasa mahospitalini bila idhini yao

Ripoti mpya iliyotolewa nchini Kenya imebaini kuwa wanawake wanaotafuta huduma za matibabu ya uzazi nchini humo wanafanyiwa ukaguzi wa sehemu za siri, kukatizwa uwezo wa kupata mimba na kufanyiwa upasuaji usiohitajika wanapojifungua, bila idhini yao.

Utafiti huo unasema, wanawake hao pia wanalazimishwa kukubali matibabu au huduma za afya ambazo hawahitaji.

Haya ni kwa mujibu wa ripoti iliyotayarishwa na Chama cha Watu wanaoishi na Ulemavu Nchini Kenya (APDK), Shirika la Kuangazia Haki za Vijana-Kenya (CAARY-AFRICA), Nguvu Collective na washirika wengine.

Matokeo ya utafiti huo yanafichua jinsi wahudumu wa afya katika kaunti 27 nchini Kenya hutoa huduma bila kuzingatia utu na heshima ya mtu.

Taarifa iliyotolewa na waandishi wa ripoti hiyo inasema: “Asilimia 68 ya visa hivyo vinakiuka haki za kibinadamu na ni vitendo vinavyowanyima wanawake haki zao za kutendewa utu na kupata huduma bora za afya wakati wa uja uzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.”

Ripoti hiyo inasema kuwa asilimia 94 ya wanawake katika kaunti hizo hawakuripoti visa vya kutendewa dhulma hizo kwa sababu hawakujua namna ya kufanya hivyo.

Aidha, ripoti hiyo inaelekeza kidole cha lawama kwa vituo vya kutoa huduma za afya ya uzazi kwa kuendesha dhulma hizo.

“Kuhusu wahudumu wa afya wanaowadhuluma akina mama, asilimia 51 kati yao ni wauguzi, asilimia 25 ni madaktari na wataalamu wa afya ya uzazi na asilimia 19 ni wafanyakazi wa vituo vya afya wasio wataalamu kama vile makarani, wadumishaji usafi, wapishi na wengineo,” inasema ripoti hiyo.

Imeongeza kuwa, asilimia 13 ya visa hivyo vina madhara ya muda mrefu kwa afya ya watoto na ukuaji wao.

Tags