Borell akosoa vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi mbalimbali
-
Josep Borrell
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amekosoa vikwazo vinavyowekwa na Marekani dhidi ya nchi nyingine vikiwemo vikwazo vya nchi hiyo dhidi ya mradi wa pili wa ujenzi wa bomba la gesi wa Russia kuelekea Ulaya wa Nord Stream 2.
Josep Borrell ametoa taarifa kali akieleza wasiwasi wake kuhusu vikwazo na vitisho vya Marekani dhidi ya makampuni na maslahi ya Ulaya na kusema: Umoja wa Ulaya unapinga utumiaji wa vikwazo vinavyowekwa na nchi moja dhidi ya makampuni ya Ulaya yanayofanya biashara halali.
Borrel ameongeza kuwa, sera za Ulaya zinaainishwa na kupangwa ndani ya Ulaya kwenyewe na haifai kuutishia upande mwingine kwa kutumia fimbo ya vikwazo.
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kutumia vikwazo nje ya mipaka ni kinyume cha sheria za kimataifa na kuongeza kuwa, tumeshuhudia mwenendo huo unaoshadidi dhidi ya Iran, Cuba, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na sasa mradi wa Nord Stream 2 na Turkish Stream.
Russia na muungano wa makampuni ya Ulaya zinatekeleza mradi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2 utakaopeleka gesi katika nchi za Ulaya, na Marekani inafanya njama za kusitisha mradi huo.