Korea Kaskazini yajiandaa kufanyia majaribio kombora jipya la balestiki
Televisheni ya Japan imetangaza kuwa, Korea Kaskazini imejiandaa kwa ajili ya kufyatua kombora jipya la balestiki.
Kanali ya NHK imetangaza habari hiyo kwa kuwanukuu wanadiplomasia wakisema kuwa, mbali na Pyongyang kujiandaa kurusha satalaiti anga za mbali, imekusudia pia kulifanyia majaribio kombora la balestiki katika mwambao wa mashariki mwa nchi hiyo.
Aidha Korea Kaskazini imetoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa kuwa, itarusha satalaiti yake ambayo itaizunguka dunia, mwanzoni mwa wiki ijayo. Uamuzi huo wa Pyongyang umechukuliwa katika hali ambayo hatua Wamagharibi wameiwekea vikwazo nchi hiyo kutokana na kujiimarisha kwa makombora.
Aidha tarehe sita mwezi uliopita Korea Kaskazini ililifanyia majaribio ya nne kombora lake la nyuklia, suala lililoibua makelele ya viongozi wa Marekani waliotaka kushadidishwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
Tayari serikali ya Pyongyang imetangaza kuwa, kuboresha mpango wake wa makombora na kutuma satalaiti anga za mbali, ni haki ya kila nchi na kusisitiza kuwa itaendelea na mpango huo.