Balozi Gharibabadi: IAEA inaruhusiwa tu kukagua shughuli za nyuklia za Iran
(last modified Fri, 11 Dec 2020 07:48:53 GMT )
Dec 11, 2020 07:48 UTC
  • Balozi Gharibabadi: IAEA inaruhusiwa tu kukagua shughuli za nyuklia za Iran

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika taasisi za kimataifa zilizoko Vienna, Austria amesema: "Jukumu pekee la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika mapatano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 ni kukagua shughuli za nyuklia za nchi hii na kutoa ripoti kuhusiana na hilo."

Balozi Kazem Gharibabadi ameyasema hayo mapema leo Ijumaa katika ujumbe alioutuma katika ukurasa wake wa Twitter katika kujibu matamshi ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuhusiana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika mahojiano yake ya kwanza baada ya kuuawa Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi wa nyuklia wa Iran, Grossi amedai kuwa,  uamuzi wa Iran wa kujiondoa katika utekelezaji wa kujitolea wa protokali ziada ya IAEA ni jambo litakalopelekea kuongezeka taharuki. Katika mahojiano na Sky News, amesema Iran haipaswi kutekeleza tishio lake la kuongeza urutubishaji urani na kuwatimua wakaguzi wa IAEA.

Shahidi Mohsen Fakhrizadeh

Akijibu matamshi hayo ya Grossi, Balozi Kazem Gharibabadi amesema kwa mujibu wa JCPOA, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hauna jukumu la kutoa tathmini au uchambuzi. Amesema majukumu ya IAEA kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA ni kukagua na kuthibitisha kuwa shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani.

Ijumaa iliyopita vyombo vya habari vya Magharibi vilichapisha habari za siri ambazo zilikuwa mikononi mwa IAEA pekee na kutangaza kuwa wakala huo ulikuwa umezipasha habari nchi wanachama kuwa Iran ilikuwa inanuia kuweka mitambo mipya ya kurutubisha urani aina ya IR-2M katika taasisi zake za nyuklia huko Natanz. Kwa mujibu wa mada ya 7 ya hati ya wakala wa IAEA, wakala huo hauruhusiwi kuvujisha habari au ripoti zozote za siri zinazohusiana na shughuli za nyuklia za nchi wanachama.

Mujtaba Zunour, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, aliashiria Jumatatu kuvujishwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA, ripoti ya nyuklia ya Iran na kusema: Wakala wa IAEA unatoa taarifa za siri za Iran kwa maadui na kutolinda amana katika hatua tofauti.

Kuuawa wanasayansi wa nyuklia wa Iran sambamba na hatua ya wakala wa IAEA ya kuvujisha taarifa na habari za siri za wanasayansi hao kunaweka wazi umuhimu wa suala hilo na ukiukaji wa wazi unaofanywa na wakala huo katika uwanja huo.